Uchungu na Msamaha – 2

Baada ya kuangalia jinsi uchungu unavyoanza hadi kukua, sasa tuone jinsi gani unaweza kuushinda uchungu kabla haujaharibu maisha yako na mahusiano yako.

Kabla hujajaribu kuung’oa uchungu inabidi ujue ni jinsi gani mizizi yake imejikita ardhini. Mizizi ya uchungu inakuwa kutoka kwenye mbegu ambayo ndiyo kosa ulilotendewa. Kosa linaweza kuwa ni tukio fulani au neno au maoni fulani au lugha ya mwili ambalo inawezekana haikukusudiwa / ilikusudiwa kukuudhi na wewe ukaona kuwa huwezi kusamehe. Usipogundua mbegu husika huwezi kung’oa mizizi yake, unaweza kata matawi na shina ila yataendelea kuchipuka hasi utakapoitambua mbegu (chanzo cha uchungu /kutokusamehe) na kung’oa mizizi yake (kusamehe).

Nguvu ya mizizi hutegemea ni kwa kiasi gani uchungu umepaliliwa na kutunzwa. Lazima mawazo yote mabaya yanayoambatana na kutokusamehe yatoke ndipo utakapoweza kuisikia sauti ya Mungu ndani ya dhamira yako inayokutaka kutubu na kuachilia. La sivyo utazidi kujiona upo sahihi na uchungu utazidi kukomaa. Lazima uachane na mawazo yanayokuonyesha wewe uko sawa na mwingine ndio mwenye makosa. Neno la Mungu lazima liingie ndani yako ili uweze kuona jinsi ambavyo Yesu anachukizwa na uchanofanya.

1) Yesu amesema tunapaswa kusamehe mara zote Mathayo 18:21-22

Usitafute sababu ya kutokusamehe, hata kama amekukosea mara nyingi Yesu ameagiza tusamehe saba mara sabini. Jifunze kuwa na msamaha wa kweli, msamaha haumaanishi kiwa hukukosewa bali unapaswa kusamehe kama ambavyo Mungu amekusamehe. Msamaha unasababisha neema ya Mungu kukaa kwa wingi ndani yako. Mume na mke lazima wasameheane katika kila hali, lisiwepo jambi ambalo mtu ataacha kumsamehe mwenzi wake. Muombe Mungu akuwezeshe kuwa na msamaha kila wakati.

2) Kisasi ni cha Mungu tu! Warumi 12:19

Kamwe usilipize kisasi. Unapojaribu kujitafutia haki kwa kulipiza kisasi unajitenga na neema ya Mungu, wewe usilipize ovu kwa ovu bali tenda mema kwa upendo. Warumi 12: 17 biblia inasema tuushinde ubaya kwa wema. Hakikisha unafanya hivyo kwa upendo ili uweze kuwaonyesha neema ya Mungu waliokukosea nao wapate nafasi ya kumrudia Mungu. Jivike upendo, utuwema, fadhili, na samehe hata kama kuna sababu ya kulaumu. Wakolosai 3: 12-13. Kamwe usiweke chuki ndani yako Wakolosai 3:8, onyesha kuwa Yesu anafanya kazi ndani yako kwa kuwa mtu wa msamaha. Kila asubuhi muombe Mungu akujalie neema yake ili uewze kuionyesha kwa watu wote utakaokutana nao kwa siku hiyo.

3) Muamini Mungu katika wakati unapoonewa Mathayo 5:10-12

Maranyingine tunajaribiwa pale ambapo watu wanatutendea visivyo. Yesu anatuamuru tupendane bila kuwa na kinyongo. Biblia inasema kuwa furahi ukiwa katika hali kama hiyo, tumia hiyo nafasi kuushinda ubaya kwa kuwaonyesha upendo. Unaweza tumia nafasi hiyo kuonyesha nguvu ya Mungu, badaya ya kuwa na uchungu samehe na pokea neema ya Mungu ya kukuwezesha kumpenda huyo aliyekukosea. Warumi 12:20-21

Mambo matatu ya kuzingatia

a) Samehe kwa moyo wako wote

b) Mtendee kwa wema na upendo ambao haustahili aliye kukosea

c) Furahi unapoonyesha upendo wa kweli kwa mtu huyo. Kwa kufanya hivyo hakika atauona upendo wa Mungu kupitia kwako.

Ubarikiwe na Bwana. Tutakuja kuangalia sasa hatua za kuondoa uchungu na kinyongo.

Uchungu na Msamaha

Uchungu ni kitu kinachoua mahusiano mengi iwe ni kifamilia, kihuduma na hata kindoa. Uchungu unaondoa ukaribu baina ya watu na kujenga ukuta wa uhasama. Uchungu unaondoa yale mazuri yote ambayo Bwana ameyaweka kwenye mahusiano yetu. Kamwe uchungu usiachwe ukakua katika maisha yetu.

Efeso 4:31 Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.

Uchungu unakuja na hasira, ghadhabu na kelele na matukano. Utakapoacha uchungu ukue ndani yako utaleta na yote hayo.

Fahamu mizizi ya uchungu inavyoanza na hatimaye kuwa shina. Uchungu unakuja pale mtu anapokukosea na wewe ukaweka kinyongo ndani ya moyo wako. Inawezekana hakukukosea kwa kukusudia lakini sababu hukutaka kumuuliza kwa upole kuhusu jambo hilo na kuamua kuliweka moyoni basi litakuletea uchungu ndani yako.

Uchungu unakuwa shina ndani yako kwa kukuonyesha kuwa uko sahihi kuwa na kinyongo kwa kosa ulilotendewa. Unapingana na dhamiri yako inayokuambia sio sawa kuwa na kinyongo na mtu. Unajikuta unawaza jinsi mtu huyo alivyokukosea na kutokuona kosa ambalo unalifanya la kuweka kinyongo na kutokusamehe.

Ebrania 12:15 mkiangalia sana mtu asiipunguke neema ya Mungu, shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.

Katika mistari hii tunaona kuwa shina la uchungu linachupuka pale ambapo mtu anakuwa ameipungukia neema ya Mungu. Mtu unapoacha kusamehe hapo ndipo unapoanzisha mizizi ya uchungu na kutokusamehe kutapelekea wewe kupungukiwa na neema ya Mungu. Unaposhindwa kusamehe wengine unakuwa unamwambia Mungu kuwa asikusamehe na ndipo unapopungukiwa na neema ya Mungu.

Unapokuwa na uchungu na mtu, sio nyie wawili tu mnao athirika bali na watu wote wanaowazunguka. Ndio maana biblia inasema tuangalie sana maana uchungu utasababisha watu wengi kutiwa unajisi sababu yetu. Shina la uchungu linachipuka kwenye mizizi ya kutosamehe, lazima ujifunze kusamehe hata kama mtu amekukosea kwa kukusudia.

Baada ya kuona jinsi uchungu unavyoanza, tutaangalia jinsi ya kuushinda. Hadi wakati huo, Ukae na amani ya Bwana.

Weka Nyumba Salama

image

Kila mtu anajisikia salama zaidi anapokuwa nyumbani kwake.Hivyo ni vizuri ukahakikisha kuwa nyumba inausalama wa kutosha kwa wote wanaoishi ndani yake kwa kuweka kila kitu mahali pake kwa usalama.

Jikoni

1. Hakikisha mikono / vishikio vya sufuria vinaelekea pembeni mbali na upande wa kupikia ambapo watu wanapita / unasimama.

2. Hakikisha sabuni zote na dawa za kufanyia usafi zipo mbali na mahali watoto wanafikia.

3. Nyaya zote za vifaa vya umeme kama birika, blender n.k ziwekwe mahali salama.

4. Watoto wasizoee kuchezea sufuria tupu maana wanawea chukua zenye moto au vitu vya moto bila kujua maana wamezoea kuzichezea.

5. Visu na vifaa vyote vyenye ncha kali viwekwe mahali salama mbali na watoto.

Bafuni

1. Hakikisha vyombo vyote vya kuwekea maji vina mifuniko inayofunga vizuri.

2. Kama baf lina ‘tiles’ weka mpira maalumu wa kusimamia ili mtu asiweze kuanguka akiwa bafuni.

3. Sabuni, dawa na vipodozi vyote viwekwe juu mbali na watoto.

Vyumbani

1. Usiweke dawa, vipodozi au hela za sarafu mahali ambapo watoto wanafikia kwa urahisi.

2. Watoto wenye umri chini ya miaka sita wasilale kwenye kitanda laini sana au chenye mablanketi mengi.

3. Nguo zote zenye kamba ziwekwe kabatini mbali na watoto. Hakikisha milango ya kabati imefungwa vizuri.

Nimekukimbilia Bwana, Usiniache Niaibike

Shalom

Zaburi 31:1-9, 14-22

Nimekukimbilia Wewe, BWANA,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye,
     Unitegee sikio lako, uniokoe hima.
Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Nyumba yenye maboma ya kuniokoa.
     Ndiwe genge langu na ngome yangu;
Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.
   Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
     Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee BWANA, Mungu wa kweli.
   Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo;
Bali mimi namtumaini BWANA.
     Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako,
Kwa kuwa umeyaona mateso yangu.
Umeijua nafsi yangu taabuni,
     Wala hukunitia mikononi mwa adui;
Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi.
   Ee BWANA, unifadhili, maana ni katika dhiki,
Jicho langu limenyauka kwa masumbufu,
Naam, mwili wangu na nafsi yangu.
   Lakini mimi nakutumaini Wewe, BWANA,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
   Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.
     Umwangaze mtumishi wako
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
     Ee BWANA, nisiaibishwe, maana nimekuita;
Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni.
     Midomo ya uongo iwe na ububu,
Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi,
Kwa majivuno na dharau.
     Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu!
     Utawasitiri na fitina za watu
Katika sitara ya kuwapo kwako;
Utawaficha katika hema
Na mashindano ya ndimi.
   BWANA ahimidiwe; kwa maana amenitendea
Fadhili za ajabu katika mji wenye boma.
   Nami nalisema kwa haraka yangu,
Nimekatiliwa mbali na macho yako;
Lakini ulisikia sauti ya dua yangu
Wakati nilipokulilia.

Usafi wa Kihisia

Kila mmoja wetu anaffahamu umuhimu wa kujitunza na kuwa safi hadi pale atakapopata mwenzi wa maisha. Kujitunza huku maranyingi huishia kwenye mwili, leo naongelea suala ambalo wengi huwa hawaligusii kabisa lakini linamadhara sana, usafi wa kihisia.

Kujitunza kwa ajili ya yule ambaye Mungu amekuandalia aihusishi kujitunza kimwili tu, bali kihisia pia. Hii inahusisha kutunza moyo wako, mawazo, maneno na macho pia. Inamaanisha kuuhifadhi ule uhusiano wa karibu wa kihisia kwa ajili ya yule ambaye Mungu amemuandaa kwa ajili yako na si mwingine yeyote. Kuepuka muunganiko wowote wa kihisia ambayo kwa kawaida ni rahisi kutokea lakini inaumiza sana kuivunja.

Usafi wa kihisia linaonekana kama ni jambo lisilowezekana katika kizazi cha sasa, lakini fikiria: Mume wako atakapokuoa atajisikiaje akijua kuwa kuna mwanaume mwingine anafahau hisia zako za ndani, malengo yako, hofu zako na mawazo yako? Atajisikiaje kujua kuna mwanaume mwingine anakufahamu vizuri kuliko hata yeye anavyokufahamu? Au utajisikiaje kujua kuwa kuna msichana alikuwa nafanya mazungumzo marefu ya hisia na undani na mume wako kabla hajawa na wewe na anamjua mume wako kiundani kabisa?

Sio tu unautunza mwili wako, kuna mambo mengi ambayo unatakiwa uyatunze kwa ajili ya mume wako pekee, yeye ndiye awe wa kwanza na wa mwisho. Wasichana wengi hawaoni umuhimu wa jambo hili, wanaweza kuwa na uhusiano wa kihisia na mwanaume ambaye hata hawanampango wa kuolewa naye na wakati mwingine mtu huyo hata hajaokoka. Hii ni mbaya sana maana ile nafasi ya kwanza ambayo anapaswa akae mume wako anakaa mtu mwingine.

Hapa siongelei sheria za kufuata ili usije ukakosea bali kuamua kujitunza na kutunza hisia zako kwa ajili ya yule tu ambaye umehakikisha kwa maombi kuwa ndiye. Kama ulikuwa na mtu, ukajua kabisa ndiye huyo na ukawa na ukaribu naye wa kihisia lakini baadaye mambo yakaja kuharibika, angalia usiingie kwenye  mahusiano na mtu mwingine hadi utakapohakikisha umemtoa kabisa kwenye moyo wako. Bila kufanya hivyo itakuja kukuletea shida kwenye uhusiano wako mpya, hii inawezekana kwa maombi na kumshirikisha Roho mtakatifu ambaye pekee ndiye anayeweza kukusaidia katika hili.

Mambo ambayo unapaswa kuyatunza na kuyafanya / kumfanyia yule ambaye unahakika atakuwa mume wako na si  mwingine yeyote ni pamoja na:

  • Maneno mazuri ya kujali na kuonyesha kumpenda
  • Kutoa zawadi au kupokea zawadi
  • Kutazamana usoni kwa mapenzi
  • Mtoko wa pamoja (outing), kumbukumbu za pamoja
  • Meseji zenye hisia za upendo
  • Kumwambia I love you / I love you too
  • Kumpa moyo wako na kumruhusu aingie moyoni mwako
  • Mawasiliano ya mara kwa mara kuelezana kila kinachotokea katika maisha yenu.
  • Kuzungumza hisia zenu za ndani, malengo, hofu, historia n.k

Bila Roho mtakatifu kutuongoza hatuwezi kuyatenda mapenzi ya Mungu, mruhusu ayatawale maisha yako na moyo wako ili uweze kuwa mshindi na zaidi ya mshindi.

Ubarikiwe na Bwana Yesu!