Mafundisho


Duniani tunapitia mambo mengi ya kuvunja moyo na kukatisha tamaa. Mengine yanaumiza sana moyo na mengine yanaonekana kutuangamiza kabisa. Lakini Bwana akiwa upande wetu tunashinda na zaidi ya kushinda. Simama na mistari hii katika yote unayopitia ukitambua ya kuwa Mungu hapendi tuteseke wala tuangamie.

OMB. 3:22-26, 31-33
“Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.    Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu.    BWANA ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye.    BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo.    Ni vema mtu autarajie wokovu wa BWANA Na kumngojea kwa utulivu.    Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele.  Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.    Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.”

Ijumaa hii ni ijumaa yetu ya maombi ya kufunga. Siku ya kukabidhi mwezi mzima mbele za Mungu na kuomba ulinzi na uongozi wake katika maisha na mipango yetu yote. Mwezi huu ni mwezi wa mwisho katika mwaka hivyo ni lazima tuutumie vizuri. Ni mwezi wa kukaa chinicna kuangalia mipango yote uliyokuwa umeipanga mwaka jana imefikia wapi, ipi imekamilika, ipi imeshindikana, ipi ipo kwenye utekelezaji na ipi ya kubadili au kufuta kabisa.

Nimeonelea kabla mwaka haujaisha tuwe na siku tano za maombi ya kufunga kwa kumshukuru kwa yote aliyotutendea mwaka mzima, kwa uzima na yote pia aliyotutia nguvu kuyakabili, kumwomba uongozi wake kwa mwaka ujao, kuomba atufunulie nini anataka tufanye kwa mwaka ujao, kuomba rehema na neema kwa makosa tuliyoyatenda na kwa uzembe wote wa mambo ya Mungu na kuomba kujazwa nguvu za Roho mtakatifu ili mwaka ujao tuweze kusimama katika zamu zetu kwa uaminifu.

Maombi yatakuwa  Kuanzia tarehe 10 hadi 14 mwezi huu.

Watu wengi tunamaswali mengi katika maisha yetu. Nifanyeje niweze kufanikiwa, nifanyeje nipate mke/mume, nifanyeje nibarikiwe, nifanyeje niweze kumtumikia Mungu n.k. Tunafahamu mwenye majibu ya maswali yetu ni Mungu pekee na humwendea na maswali haya ili kupata majibu. Cha kushangaza hatutaki kusikia majibu yake bali tunataka majibu ambayo tunayataka!!

Unapomwendea Yesu kutafuta majibu ya maswali yako uwe tayaru kupokea majibu yake. Kama hautaki kuyapokea majibu toka kwa Mungu sawasawa na mipango yake kwako haina haja kupoteza muda kuomba. Tunakuwa kama yule tajiri aliyemuuliza Yesu afanye nini ili aweze kuurithi ufalme wa mbinguni, alipoambiwa auze vyote na kuwapa masikini halufurahishwa na akaondoka kwa huzuni.

Kama unaamini Mungu ndiye mwenye majibu ya maswali yote, kuwa tayari kuyapokea majibu toka kwake maana yeye anaujua mwisho wetu kabla ya mwanzo na anatuwazia mema siku zote.

Mwanzoni ulikuwa ni mtu mwenye kumpenda Mungu sana. Ulikuwa mwenye bidii katika mambo yote ya Mungu, maombi, kujifunza neno, kushuhudia na ulijiweka mbali na dhambi. Haikuwa kazi kukataa mambo ambayo unajua hayampendezi Mungu. Kila mtu alijua jinsi unavyompenda Mungu na hawakuweza kuongea au kufanya yasiyofaa mbele yako.

Lakini sasa upo mbali sana na Mungu. Mwenyewe unashangaa ni nini kimetokea, huna kabisa shauku na mambo ya mungu kama mwanzo. Unatamani sana urudie hali ya mwanzo lakini umeshindwa. Roho yako inahangaika lakini mwili haupo radhi kabisa. Mambo ambayo mwanzoni ulikuwa huwezi kuyafanya sababu ni machukizo mbele za Mungu siku hizi hata hujifikirii mara mbili kabla ya kuyafanya.

Mungu bado anakupenda. Anakuita kwa upendo urudi kwake. Tazama ni wapi ulianguka, ugeuke, ukatubu na uanze upya na Yesu. Mwanampotevu alipogundua kosa lake hakuona aibu, alirudi kwa baba yake na kuomba msamha. Rudi kwa Mungu wako, anza upya na Bwana. Bwana yupo mlangoni anakusubiri, macho yake amekaza kuangalia njia uliyotokea alikuw kuwa utarudi. Usione aibu, Rudi kwa baba yako.

Usiku hujalala sababu ya uchungu mwingi na matatizo mengi. Umelia usiku kucha lakini bado hakuna badiliko. Umeamka sababu huwezi kulala siku nzima lakini hukutaka kabisa kuamka. Umeenda kazini kutimiza wajibu lakini moyo na mwili ni mzito kabisa. Unacheka lakini moyo unalia na kusononeka. Umefika hatua ya kukata tamaa na kuvunjika moyo kabisa na huoni faida ya kuishi.

Katika yote hayo kumbuka kuwa yupo mfariji. Mfariji wa ajabu ambaye hujishughulisha sana na mambo yetu. Mfariji ambaye ukimuita atakuwa nawe muda wote kukupa amani, furaha na tumaini la kweli. Matatizo unayoyapitia leo siku moja hutayaona tena, kama ambavyo wana wa Israel hawakuwaona tena wamisri pale Bwana alipowatoa chini ya utumwa wao. Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya.

KUT. 14:13-15
“Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.  BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.”

Watoto wetu wanapitia hatari nyingi sana katika maisha yao. Matatizo ya watoto katika kizazi hiki ni mengi sana nasi wazazi hatuna nguvu ya kuwalinda na hayo yote zaidi ya kumwita Mungu. Wiki hii tunaenda kuomba kwa ajili ya watoto wetu, ajali za majumbani, ajali za shuleni, unyanyasaji wa kila aina, magonjwa, kiburi, utukutu, marafiki wabaya, kutokupenda shule, kushindwa kusoma, nguvu za giza na mengine meeengi.

Tumlilie Mungu kwa ajili ya watoto wetu, na kuwakabidhi mbele za Mungu. Hakuna awezaye kuwalinda na kuwalea watoto bila msaada wa Mungu.

Kuna mtu aliniandikia message analalamika kuwa maisha yake yamekuwa ni ya mateso matupu, amekuwa mtu wa kuhangaika kwenye nyumba za watu mara leo anaishi na huyu mara na yule na anaona kuwa amezaliwa ili apate shida. Nilimtia moyo na kumpa maneno ya kumsaidia. Ila nimeona leo niliongelee jambo hili hapa.

Watu wengi sana wanasumbuliwa na hali ya kukosa shukurani. Ukimwambia mtu hivyo anaruka hapana mimi naahukuru kwa kila ninalopewa, ila ukweli unabaki kuwa tatizo hili linasumbua wengi. Na linaongezewa na hali ya kuona kuwa mtu mwingine ndiye anajukumu la kukupa furaha na kufanikisha maisha yako mfano mzazi, ndugu, rafiki, mume, mke n.n.

Nilikutana na mtu aliyenifundisha jambo kubwa sana kutokana na maisha yake,. Niliposikia habari za maisha yake nilijua nikikutana naye atakuwa mtu mwenye kusononeka, huzuni, anayejiurumia na kulaumu wengine lakini haikuwa hivyo. Alikuwa mtu aliyejaa furaha, mkarimu, anayepambana kuyakomboa maisha yake bila kuangalia changamoto lukuki zilizomzunguka na anayewajali na kuwasema vizuri wale ambao kwa uhakika walistahili kumsaidia lakini walimtenga.

Nikajjfunza kuwa hata ukijuhurumia na kulaumu mazingira yaliyopelekea hali yako kuwa hivyo kamwe huwezi kuibadili, unapaswa kumshukuru Mungu kwa vile ulivyonavyo na kiwela bidii, narudia bidii ili kuyakomboa maisha yako. Usiishie kuota, bali fanya kazi kwa uwezo wako wote. Mshukuru Mungu una watu wanaoweza kukupa mahali pa kulala hata kama ni wiki moja, mshukuru Mungu unapata chakula kuna ambao hata hizo nyumba za kuzunguka leo kwa huyu kesho kwa huyu hawana. Changamoto zako ziwe daraja la kukuvusha kuelekea mafanikio na sio utelezi kukupeleka shimoni.

« Previous PageNext Page »

Follow

Get every new post delivered to your Inbox.

Join 163 other followers