
SOMO: HANA – UTHABITI KATIKA MAJARIBU
MAANDIKO: 1 SAMWELI 1:1-28; 2:1-10
Hana alikuwa ameolewa na mtu aitwaye Elikana. Elikana alikuwa na wake wawili wa kwanza akiitwa Penina na wa pili Hana. Penina alikuwa amejaliwa watoto wa kike kwa wa kiume lakini Hana yeye hakuwa na mtoto. Hali hiyo ilikuwa inamuumiza sana, mumewe alijitahidi kumuonyesha upendo na kujali ila bado moyo wake ulikuwa na mzigo mkubwa. Penina hakuwa msaada bali alizidisha maumivu ya Hana kwa kumchokoza kwa sababu ya kukosa mtoto.
Hali hiyo ya maumivu ya kukosa mtoto na kuchokozwa ilimpelekea Hana kuwa na maombi mazito mbele za Mungu. Hapa tunaona jinsi Hana alivyokuwa mwanamke thabiti wa imani, alikuwa na kila sababu ya kulalamika na kuona kama Mungu amemsahau au kuingia kwenye malumbano na Penina. Yeye alitambua kuwa mwenye uwezo wa kumpa mtoto ni Mungu na kamwe hawezi kushindwa, aliingia kwenye maombi na kukazana na maombi akiamini Mungu atafanya. Alimwekea Mungu nadhiri kuonyesha ni jinsi gani anahitaji mtoto.
Tunaona pia akiwa kwenye maombi mazito hadi sauti ikawa haitoki, kuhani Eli alidhania amelewa. Unaweza ukaona ni jinsi gani Hana alikuwa anaomba kwa uchungu, na alijisikiaje vibaya baada ya kuhani kuanza kumgombeza kuwa atalewa hadi lini wakati yupo kwenye majonzi mazito. Lakini majibu yake yanaonyesha kuwa Hana hakuruhusu maneno yale yamuondoe kwenye kusudi la maombi yale, hakuruhusu maneno yale ya kukatisha tamaa yaweke uchungu ndani yake bali aliendelea kuwa mnyenyekevu akimwamini Mungu. Unaweza kuwa unapitia magumu sana katika maisha halafu wale unaowategemea wakutie moyo na kukufariji ndio wakawa wa kwanza kukutuhumu na kukulaumu.
Tujifunze kwa Hana, usiyaweke moyoni maneno hayo wala usikubali yakutoe kwenye maombi yako kwa Mungu. Vile vile hapa tunaona shutuma za Eli hazikumfanya Hana amuone hafai na kutokumsikiliza. Aliendelea kumheshimu kama kuhani na alisikiliza neno lake na kulifanyia kazi. Wengi wetu hapa tungeshindwa. Tujifunze kwa mwanamke huyu mwenye imani thabiti. Endelea kumwamini Mungu, endelea kumimina moyo wako mbele za Mungu na hakika wakati utawadia na Bwana atatenda kwa utukufu wake. Wakati wa Bwana utawadia tu, Bwana mwenyewe atawanyamazisha wanaokushutumu na kukuchokoza kwa sababu ya hali uliyonayo. Usitafute wewe kuwanyamazisha, tujifunze kwa Hana alivyokabiliana na Penina bila kujibizana naye.
1 Samweli 1 : 20 – Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.
Pia tunaona kuwa Hana alikuwa mwaminifu kumtolea Mungu nadhiri aliyoiweka. Pamoja na kuwa alihitaji mtoto sana lakini hakuacha kumpeleka hekaluni kama alivyoahidi kwenye maombi. Unapokuwa katika maombi kama huna uhakika na uwezo wa kuitumiliza nadhiri ni vena usiiweke. Uwekapo nadhiri yako kwa Mungu hakikisha umeiondoa pale Mungu anapo kutendea.
Kumbukumbu la Torati 23 : 21 – Utakapoweka nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.
Mhubiri 5 : 4 – 5 Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri. Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe.
Tunamaliza somo letu kwa wimbo wa sifa kutoka kwa Hana. Hana alimwomba Mungu kwa machozi na alipotendewa alirudi na wimbo wa shukrani. Je umemshukuru Mungu kwa yale amekutendea au unaona ni sababu ya maombi yako mengi na mazito ndio maana umepata? Ukisoma sura ya pili hapo utaona shukrani zake kwa Mungu. Ameonyesha kabisa kuwa ni Mungu tu aliyetenda na mwenye nguvu, yeye hana la kujisifia. Tujifunze katika hili.
Maswali
1. Nini kilimpa Hana uchungu mwingi? Je ni maneno ya Penina.? Shutuma za Kuhani? Kutokuwa na mtoto?
2. Alikabiliana vipi na maumivu na uchungu ndani yake?
3. Unadhani ilikuwa rahisi kukabidhi mtoto kwa kuhani baada ya kumsubiri kiasi hicho?
4. Ni kiasi gani maneno ya watu ya kukatisha tamaa na kuvunja moyo yamekuathiri na kukuzuia kufikia ndoto zako?
5. Pale Unapokuwa na hitaji kubwa ila hauoni kama linapatikana huwa unakabiliana vipi na hali hiyo?
6. Je pale kiongozi wako wa imani anapokuonyesha kutokuamini unayoyafanya na kukushutumu huwa unakabiliana vipi? Je huwa unaendelea kumsikiliza akisema maneno ya Mungu?
7. Umejifunza nini kupitia maombi ya shukrani ya Hana?
Limeandaliwa na womenofchrist.wordpress.com