Mungu Bado ni Mungu Hata Nyakati za Shida

Wakati unapokuwa katika hali nzuri, mambo yako yanaenda kama ulivyopanga, kila kitu kwenye maisha yako kipo kwenye mstari, upo kwenye kilele cha furaha na mafanikio ni rahisi sana kuwatia moyo wengine, kukiri ukuu wa Mungu, kuongea maneno ya kuinua na kuamini kuwa Mungu atakuinua zaidi na zaidi. Ahadi za Mungu unaziona ni zako.

Lakini pale unapokuwa chini, kila unaloshika linafeli, mambo yako yote hayana muelekeo, kila upande ni madeni, magonjwa, shida na matatizo… Inakuwa Mungu sana kuliamini neno la Mungu. Ahadi za Mungu unaziona kama wewe zimekuruka. Unaona kama vile Mungu hayupo, amekuacha na hata mtu akikutia moyo unaona anaongea tu na yale uliyokuwa unayakiri mwanzo sasa unaona kama haiwezekani.

Nakutia moyo mpendwa, haijalishi hali gani unayopitia, Mungu bado ni mwaminifu na ni yeye yule hajabadilika kamwe. Mungu wa wakati wa raha bado ni Mungu hata wakati wa shida, Mungu aliyekufanikisha bado ni Mungu hata ukipita katika magumu, Mungu aliyewavusha wana wa Israel bahari ya shamu bado alikuwa Mungu  wakati wa vita. Hakika hatakuacha wala kukupungukia. Usiache kumuamini nyakati zote.

Mwanamke Usikate Tamaa Katika Majaribu

Wanawake kwenye ndoa wanapitia mitihani na majaribu mengi sana. Majaribu haya yapo katika kila hatua ya maisha na ni hakika ya kuwa mengine ni mazito sana na yanaumiza sana. Kuna majaribu ya kukosa mtoto, moyo unasononeka na ndugu wanakusimanga; Majaribu ya magonjwa kwa watoto, wengine watoto wanahitaji uangalizi maalumu hivyo huwaumiza sana; majaribu ya uzazi, kuanzia mimba hadi kujifungua nayo huumiza sana mwili.

Yako pia majaribu yanayoletwa na ndugu na jamaa, wakwe kwa wifi, yani wanaamua tu kutokukukubali, kukutafutia visa na kukuumiza. Mengine ni ya kipato, mambo yanayumba, ada za watoto zinakosekana, maisha yanakuwa magumu sana; bado hujakutana na ya wasichana wa kazi. Kubwa zaidi wengine jaribu lao kubwa ni mume, anaweza kuwa hamsikilizi, hamshirikishi mambo yake, sio mwaminifu, mkorofi n.k.

Pamoja na hayo yote mwanamke hupaswi kukata tamaa, hupaswi kuacha tu, unatakiwa kupambana, kusimama katika zamu yako, na kuomba kwa bidii. Ndoa nyingi zimesimama leo hii sababu ya ujasiri na moyo wa kutokukata tamaa wa nwanamke. Sio kosa lako mambo yamekuwa kama yalivyo, hivyo hakuna sababu ya kujilaumu bali Simama na Mungu, fanya yale ya nafasi yako na furahia maisha bila kuishi kwa unyonge kutokana na majaribu.

Mungu atakupa uwezo wa kuyashinda, Mungu atakupa mlango wa kutokea.

1 KOR. 10:13 SUV
“Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”

Mwanamke ni Jeshi Kubwa

Shalom wana wa Mungu
Furahia kuzaliwa mwanamke, Mungu anakuthamini sana. Usikubali udanganyifu kuwa mwanamke ni mtu wa asiye na uwezo. Mungu alitambua kuwa dunia inahitaji mwanamke ili mwanaume aweze kuishi vizuri ndipo akasema si vyema mtu huyu awe peke yake.

Tangu agano la kale tumeona jinsi ambavyo Mungu amewatumia wanawake kutimiza mambo makubwa mfano Jeochebedi aliyemtunza Musa asiuwawe, nabii Debora aliyekuwa jasiri, Rahabu mkarimu aliyewahifadhi wapelelezi, Ruth kwa upendo aliyemtunza mkwe wake Naomi baada ya watoto wake wote wa kiume kufariki, Abigail kwa hekima na ukarimu aliyemzuia Daudi kufanya mauaji mkubwa, Mjane wa serepta aliyemlisha nabii Eliya, mwanamke mshunami aliyempa Eliya mahali pa kuishi.

Wengine ni Mariamu Magdalena na wanawake wengine waliombatana na Yesu siku zote wakiwahudumia wanafunzi na hata wanafunzi walipomkimbia msalabani wanawake hawa hawakumuacha hadi kaburini, Lydia aliyewatunza na kuwahudumia mitume n.k.n.k

Mifano yote hii inatuonyesha kuwa mwanamke akisimama katika zamu yake katika kanisa la Mungu mambo mkubwa yanafanyika. Usijidharau wala kudharau kile Bwana ameweka ndani yako. Mtumikie Bwana kwa uaminifu na hakika Mungu ataonekana, iwe ni kwa familia, wageni, watumishi wa Mungu au ni taifa, Simama ukatende.

Mfuate Mungu Kikamilifu

Ifike wakati uamue kuwa upo upande gani. Watu wengi siku hizi wanasema wanampenda Mungu lakini bado hawataki kumfuata Mungu kikamilifu. Katika magumu wapo mstari wa mbele kukiri ukuu wa Mungu ila pale maisha yanapokuwa mazuri hawataki kabisa kufuata neno la Mungu. Huku unaenda kanisani ila bado uzinzi unaufanya, pombe unakunywa, rushwa unapokea na udanganyifu mwingine mwingi unaufanya.

Biblia inasema hauwezi kuwatumikia mabwana wawili, Leo kanisani kesho upo disco, Leo kwenye maombi kesho kutoa rushwa, Leo unakiri ukuu wa Mungu kesho unatafuta jinsi ya kulipiza visasi na kumkomoa fulani, Huku unamlilia Mungu kwa maombi, usiku unakunywa vilevi. Chagua hivi leo utakaye mtumikia, kama ni Mungu au shetani na nafsi yako. Mungu anasema uwe moto au baridi, ukiwa vuguvugu atakutapika. Geuka leo ukaifuate njia ya uzima katika ukamilifu wake na uache michanganyo.

UFU. 3:15-16, 19
“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.”