Wazazi Jukumu Lako la Kwanza ni Watoto Wenu

Wazazi wanajukumu kubwa la kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao ya kila siku na kuwaandalia maisha bora ya baadaye. Mume unajukumu la kuhakikisha familia yako inapata mahitaji yote muhimu na kuwahakikishia maisha ya baadaye. Mume na mke kwa pamoja lazima mhakikishe mnapanga Mipango yenu na mapato yenu kuandaa maisha mazuri kwa watoto wenu hasa malazi, chakula, matibabu na elimu.

Ni jambo lisilokwepeka kuwa pamoja na familia zetu tuna ndugu ambao wanahitaji msaada wetu lakini mzazi/ mume/mke lazima uwe makini sana unapotoa msaada. Tambua kuwa priority yako ni familia yako na usifanye jambo ili uonekane kuwa ni mtu mwema na mkarimu kwa ndugu huku ukiiacha familia yako kwenye matatizo. Tunapotoa kwanza tuhakikishe familia zetu zina basic needs. Wazazi wetu ni priority maana kama sio wao tusingefika tulipo na hatupaswi kuwasahau kabisa ila unapotaka kusaidia ndugu wengine kaa chini na mke wako, wekeni mipango yenu na mapato yenu chini mfanye analysis kuona kama mnauwezo wa kusaidia au la bila kuhatarisha kesho ya watoto wenu.

Kumbuka kuwa leo utakapokuwa unatumia kila ulichonacho kusaidia kila ndugu uliyenaye, kesho mambo yakaenda ndivyo sivyo na watoto wako wakakosa mahali pa kuishi wakati leo uwezo wa kuwatafutia unao wewe unazitoa tu, hao hao ndio wataanza kukucheka kuwa hauna mipango ya kueleweka na hujui kutunza familia yako. Siku ukistaafu huna nyumba yako, hao hao watakucheka umechezea muda na hela yako na wala hawatakumbuka kuwa ulizitumia kwao. Toa msaada, saidia ndugu zako ila tumia akili na busara kwanza. Hakikisha misaada yako haiathiri watoto wako na maisha yao yajayo.

Advertisements

Misingi ya Ndoa: Mume Kumpenda Mke

EFE. 5:25-26, 28-31
“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.”

Ni ukweli usiopingika kuwa mwanamke anapaswa kumtii mume wake. Wanawake wamekuwa wakifundishwa kila siku kuhusu utii kwa mume, tangia wakiwa wasichana. Wanawake wengi kwenye ndoa wanapata taabu sana maana waume zao wanashindwa kabisa kuwaonyesha upendo wakati mwingine kwa kutokujua au kwa makusudi. Hali hii imewafanya waonyeshee utii kwa kujilazimisha na kwa hali ngumu lakini kama mume angefahamu kuwa mke anastawi kwa kuonyeshwa upendo na akamuonyesha upendo ndoa nyingi sana zingepona na kuona furaha ya ndoa.

Biblia iko wazi sana kuhusu jambo hili na imelinganisha upendo wa mume kwa mkewe kama upendo wa Kristo na kanisa, na mume anapaswa ampende mkewe kama mwili wake mwenyewe.
Mume unawezaje kumpiga mke wako? Hivi kweli mtu unaweza kuupiga mwili wako mwenyewe? Unawezaje kumpuuza mke wako? Unafanya mambo bila kumshirikisha, hautambui mchango wake katika maendeleo na ustawi wa familia? Unawezaje kumtelekeza mke wako? Kumsimanga na hela ya matumizi? Kumuonyesha mke upendo sio udhaifu, sio kutawaliwa wala sio kujishusha bali ni kuonyesha jinsi gani wewe unasimama na neno la Mungu.

Mke ni msaidizi, mke ni ubavu wako, mke ni sehemu yako, mke ni mwili mmoja na wewe hivyo basi usimuone kama adui yako, mshindani wako, mtumwa wako wala mtu wa kukutumikia bali awe rafiki yako, mshauri wako, mtu wako wa karibu na sifa yako.

Mume Kumjali Mkewe

Wanawake wamekuwa wakilalamika kuwa wanaume wengi wa ki Africa hawako romantic yaani hawawezi kufanya mambo ya kuonyesha upendo kwa wake zao mfano kumfungulia mlango wa gari, kumsogezea kiti akae wakiwa restaurant au hata nyumbani, kumsaidia mizigo wanapokuwa supermarket, kumnunulia maua au zawadi ndogo ndogo, kumuandalia kikombe cha chai au glass ya juice siku anapokuwa down au amechoka na kazi fulani na mengine kama hayo.

Lakini pia ukiangalia upande wa pili jamii na hasa wanawake wenyewe tunachangia hali hii, mtu akiona kaka yake anamfanyia mkewe mambo kama haya basi ataanza maneno ooh kaka ameolewa, ooh kaka hafurukuti kwa mkewe, mara limbwata n.k. yaani hata watu wakiona mtumishi wa Mungu anamfanyia mkewe basi wataona yule mama hana heshima kwa mumewe. Hii inawafanya wanaume waone kuwa kufanya hivi sio sawa wakati ni mambo yanayoongeza na kuchochea upendo. Yaani unaweza kuona wata familia wakiwa outing ni mama tu anayehangaika na watoto mara bembea mara kuogelea mara huku mara kule, baba akiwa anahangaika nao mama amekaa na rafiki zake wanapiga story utasikia Mmh mwanamke huyu hafai…

Jamii lazima ifike mahali itambue kuwa mke ni msaidizi wa mume na sio mtumwa, mke ni sehemu ya mume, ubavu wake na anastawi mahali penye upendo wa hali ya juu. Mume ampende mkewe kama Kristo alivyolipenda kanisa, upendo wa kujitoa, upendo usio na kipimo, upendo usiotafuta sababu, upendo usioangalia makosa, upendo wa kumuwazia mema siku zote, upendo wa kujali na upendo wa kutunza.

Changamoto kwetu sote…!

Panda kwa Machozi Utavuna Kwa Furaha

ZAB. 126:5-6
“Wapandao kwa machozi Watavuna kwa kelele za furaha.  Ingawa mtu anakwenda zake akilia, Azichukuapo mbegu za kupanda. Hakika atarudi kwa kelele za furaha, Aichukuapo miganda yake.”

Kupanda siku zote ni kazi ngumu. Kwanza ni lazima uamke asubuhi na mapema, ubebe mbegu na jembe, utembee kwenye baridi kuelekea shamba ambalo limejaa matope maana watu hawapandi wakati wa kiangazi, uiname shambani siku nzima au siku kadhaa ukipanda mbegu zako. Sio zoezi la kufurahia au kuchekelea lakini ni la muhimu sana kama unataka kuvuna.

Siku ya kuvuna ni siku ya furaha, siku ya kuhesabu utajiri, siku ya kuhesabu matunda ya jasho, siku ambayo taabu ya kupanda inazaa matunda, pamoja na kwamba utachoka lakini unakuwa umejaa furaha maana sasa mavuno umeyapata. Lakini huwezi kuvuna bila kupanda, lazima upande ili utazamie kuvuna. Usione wengine wanapanda ukavuta shuka halafu ukasubiri nawe ukavune.

Leo nakutia moyo wewe uliye kwenye hatua ya kupanda, Usikate tamaa jua ipo siku utavuna kwa kelele za furaha. Unaweza kuwa unapanda kwenye elimu, biashara, ujasiriamali, ufugaji kazini kwako, uwekezaji, ujenzi, huduma n.k. wewe endelea kupanda kwa bidii, panda mbegu nyingi kadiri uwezavyo wala usiwe mvivu. Mbegu siku zote ni chache na mavuno ni mara 100, hivyo panda, panda, panda. Na wewe unayesubiri kuvuna wakati hutaki kupanda kwa machozi tambua kuwa hakuna kuvuna bila kupanda. Ukitaka siku ya mavuno nawe ushangilie chukua mbegu shika njia nenda shambani ukapande.
Mbarikiwe.

Mungu Atakupigania na Adui Zako

Wana wa Israel waliteseka kwa miaka mingi katika nchi ya utumwani misri. Walimlilia Mungu kwa muda mrefu, na wakati wa Bwana ulipofika Mungu akashuka na kuwaokoa.

KUT. 3:7-9
“BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.”

Baada ya Bwana kuwatoa misri bado farao aliwafuatilia, lakini muda wa Bwana kuokoa ukifika hakuna awezaye kuzuia. Bwana aliteketeza jeshi lote la wamisri baharini na kuwaokoa watoto wake.

KUT. 14:13-15, 25
“Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.  BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa BWANA anawapigania, kinyume cha Wamisri.”

Bwana atakupigania kinyume na adui zako wawe ni magonjwa, kukataliwa, kukosa kazi, kukosa mtoto n.k. Simama katika imani ukauone wokovu wa Bwana.

Mistari ya Faraja Unapojaribiwa

Mistari ya Biblia ya Faraja unapopata miscarriage au jaribu lingine lolote…

YER. 17:7-8
“Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake.    Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.”

OMB. 3:24-26
“BWANA ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye.    BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo.    Ni vema mtu autarajie wokovu wa BWANA Na kumngojea kwa utulivu.”

KUM. 31:6
“Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana BWANA, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”

ZAB. 28:7-9
“BWANA ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru.  BWANA ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi wake.  Uwaokoe watu wako, uubariki urithi wako, Uwachunge, uwachukue milele.”

ZAB. 27:14
“Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.”

ZAB. 55:22
“Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.”

ISA. 41:10
“usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”

Mungu wa mbinguni akufariji, kukutunza na kukuhifadhi katika pendo lake. Usikate tamaa wala kuvunjika moyo, hao waisrael unaowaona leo hautawaona tena milele, Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya.

Majaribu ni Kipimo cha Imani

Miscarriage ni jambo linaloumiza sana. Linaumiza zaidi iwapo litatokea zaidi ya mara moja. Mungu anapoweka mtoto ndani ya tumbo la mama tayari kunakuwa na muunganiko kati ya mtoto na mama sasa yule mtoto anatoka kabla ya muda kufika humuacha mama na simanzi na majuto sana. Anahangaika, anajiuliza why me, analia usiku na mchana na mbaya zaidi jamii haioni kama jambo hili ni kubwa kiasi gani kwa mama na hivyo badala ya kumtia moyo wanazidi kumuumiza. Maneno kama ‘mbona ni jambo la kawaida’, ‘usijali utapata mwingine bado mdogo sana’,’mtoto wala hujamuona hivyo haukumzoea hivyo haiumi sana’,’ulikuwa unafanya kazi sana’,’ni kosa lako’ n.k. huzidisha maumivu na wala hayasaidii kabisa, ni bora ukampa maneno ya Mungu yenye uwezo wa kufariji, kuponya na kuhuisha.

Majaribu kwa mtu wa Mungu ni kipimo cha imani, tunapitia majaribu mbalimbali kila siku. Kuanzia kwenye afya, watoto, kazi, biashara, ndugu, huduma n.k na majaribu haimaanishi kuwa wewe ni mtenda dhambi au Mungu hasikii maombi yako. Shetani aliruhusiwa kumjaribu Ayubu maana Mungu alikuwa anajivunia mtumishi wake kuwa ni mkamilifu na mwaminifu na hawezi kumuacha Mungu katika hali yoyote atakayopitia. Ayubu alipitia majaribu makubwa sana kuanzia mali, watoto, marafiki ndoa na afya yake lakini hakumlaumu Mungu wala kumuwazia mabaya bali alijua kuwa katika hali yoyote bado atamuona Mungu maana ametunza uaminifu wake. Mtetezi wako yu hai na hakika atasimama kukutetea, haijalishi unapitia mangapi na makubwa kiasi gani, simama na Yesu na usimuache maana yeye hajakuacha.

AYU. 1:1, 8
“Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.”

AYU. 19:25-27
“Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.  Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu;  Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu!”

AYU. 42:2, 12
“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.  Basi hivyo BWANA akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu.”