Mavazi na Urembo


image

Pochi ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanamke. Pochi zipo za aina, rangi, ukubwa na matumizi mbali mbali. Ni nadra sana kukutana na binti au mama anayetembea bila pochi, na kwa wengine maisha yao yote wanatembea nayo kwenye pochi.

Kuna vitu muhimu ambavyo ni lazima kila mwanamke akumbuke kutembea navyo kwenye pochi, na kuna vingine ni vyema kuwa navyo lakini sio lazima.

Muhimu

1. Pini
2. Sindano na uzi
3. Vifungo
4. Dawa yoyote ambayo unaitumia na kuihitaji
5. Kitambulisho
6. Pedi
7. Kalamu na notebook

Ukipenda

1. Perfume
2. Lip shiner / lip stick
3. Poda
4. Kitana
5. Khanga / mtandio
6. Kadi ya benki
7. Sandals kama unavaa viatu virefu

Mara nyingi wanawake tumekuwa tukijichukia na kujiona si wazuri wala hatupendezi kwa kuangalia muonekano wa nje. Unajiangalia na kujilinganisha na wengine na kuishia kuona mabaya (usiyoyapenda) na kuacha kuona jinsi Mungu alivyokuumba vyema na kukubariki. Utaona kuwa hauna nywele nzuri kama fulani, umenenepa/ kukonda sana, hauna elimu kama wengine, haujaolewa na mengine mengi.

Tambua hakuna mwanadamu aliye mkamilifu bali Yesu Kristo Bwana wetu ndiye atukamilishaye. Hivyo ulivyo ni wa thamani sana mbele zake na anakuhitaji uache kuangalia madhaifu yako bali umwangalie yeye ili aweze kukutumia. Jenga tabia ya kuhesabu baraka zako kila siku na utaona jinsi maisha yako yatakavyo badilika. Jione vile Mungu anavyokuona na acha kutumia vipimo vya wanadamu kutambua thamani yako.

Hivyo ulivyo Mungu anataka kukutumia, kwa elimu uliyonayo, kazi uliyonayo, nafasi yako hiyo hiyo uliyonayo, Mungu anakuhitaji. Unaweza kudhani kuwa ungekuwa na elimu zaidi, nafasi kubwa zaidi kwenye jamii, umeolewa, unakarama kama ya fulani basi ungemtumikia Mungu. Ukweli ni kwamba hivyo ulivyo unahitajika shambani mwa BWANA, kwa karama aliyokupa (kila mmoja wetu amepewa, nitafundisha juu ya hili siku zijazo). Anza sasa kumtumikia Mungu na utaona jinsi gani utabarikiwa na kuinuliwa zaidi na zaidi.

1 Korintho 15:10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.”

1Samweli 16:7 Lakini BWANA akamwambia Samweli, usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje,bali BWANA hutazama moyo.

Mungu pekee ndiye anayeweza kuuona moyo wa mwanadamu, mwanadamu hawezi kuona moyo hivyo yeye yupata majiby yake pale anapoangalia mwonekano wa nje. Kutokana na hili basi ni vema wanawake wa kikristo tukawa na muonekano mzuri ili uwe ushuhuda mwema kwa wale wanaotutazama. Moyo mnyenyekevu na mwema huonekana katika muonekano wa nje, ni vyema tukajitahidi kuvaa vizuri, nadhifu na maridadi bila makwazo wala kujishushia thamani.

Muonekano mzuri ni muhimu sababu wewe ni kielelezo kwao waaminio na kwa wale wasioamini na kwa familia yako pia. Kwa wale walioolewa hakikisha muonekano wako haumfanyi mume wako akakosa heshima, vaa vile mume wako anavyopendezwa kuliko kuvaa ili kuwapendeza watu wengune.

2 Korinto 11:7b..Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume.

Pia kumbuka kuwa muonekano wako unaonyesha jinsi ulivyo, kama upo rafu rafu basi inaonyesha kuwa hata katika mambo yako mengine haujali, haipendezi mdada kwa na nywele zimefumuka au kuchakaa bila kuzitengeneza vizuri, au kuvaa nguo inayoonyesha sehemu kubwa ya mwili wako mfano kifua, mgongo au mapaja. Kwanza unajivunjia heshima na kumdharaulisha Mungu wako wa wale wanaokuona.

Vaa nguo inayokutosha vizuri, sio kubwa sana sio ndogo sana, hakikisha nguo ipo katika hali nzuri, sio unavaa sketi zipu imefungwa na pini au blauzi isiyo na baadhi ya vifungo. Pia ujue nguo ipi ni ya kuvaa mahali gani na kwa wakati gani, sio nguo ya kwenye sherehe ya usiku wewe unaivaa kanisani. Jitahidi kuuweka mwili wako katika hali nzuri, usiwe na harufu ya jasho wala nywele zisiwe na harufu yoyote mbaya. Tunza mwili wako maana ni hekalu la Roho mtakatifu. Jipende kwanza mwenyewe ili watu wengine nao waweze kupendezwa nawe.

Ubarikiwe.

Mikono ni mojawapo ya sehemu muhimu katika mwili wa mwanamke. Mikono hutumika kufanya shughuli zote za nyumbani kuanzia kupika, usafi, malezi n.k na isipotunzwa vizuri ni rahisi sana kuharibika na kupoteza mvuto wake wa asili. Urembo wa mikono sio lazima ufanyike saluni au kwa wataalamu, wewe mwenyewe unaweza kufanya hivyo kwa muda wako kwa gharama nafuu.

Vitu Vinavyohitajika

 • Pamba ya kutolea rangi kama umepaka rangi
 • Dawa ya kutolea rangi
 • Mashine ya kukatia kucha au mkasi mdogo
 • Tupa ya kucha (Nail file)
 • Brash ndogo ya mikono
 • Sabuni ya kunawia
 • Rangi ya kucha kama utapendelea

1.Kwa kutumia pamba na dawa ya kutolea rangi toa rangi yote kwenye kucha na hakikisha imetoka kabisa.

2. Kata kucha zako kwa urefu unaoutaka kwa kutumia ‘nail cutter’ au mkasi mdogo.

3. Lainisha ncha za kucha zako kwa kutumia tupa ya kucha, hakikisha unazisugua kuelekea upande mmoja ili kuepuka kucha kuvunjia. Kusugua kwa kwenda mbele na nyuma husababisha kucha kuvunjika upesi.

4. Kwa kutumia maji ya uvuguvugu na sabuni laini pamoja na brashi ndogo ya mikono, osha mikono yako vizuri na kuisugua  hasa sehemu za kucha.

5. Kausha mikono yako vizuri kisha paka losheni, hakikisha umepaka hadi kati kati ya vidole.

6. Kama utahitaji kupaka rangi, chukua pamba na remover na kutoa mafuta kwenye kucha zako kisha anza kwa kupaka rangi ya maji mpako mmoja na ikisha kauka ndipo upake rangi uliyoikusudia. Paka mpako wa kwanza acha ikauke kisha paka mpako wa pili na ukishakauka malizia na rangi ya maji ili kung’arisha na kuleta mvuto zaidi.

Tip: Kama kucha zako zimebadilika rangi kutokana na kupaka rangi mara kwa mara, loweka mikono yako kwenye maji yenye limao kwa dakika 5.

Kama hauna tupa ya kucha unaweza kutumia kiberiti ule upande wenye baruti.

Urembo na Mapambo

 • Bangili, hereni na mikufu unayoitumia mara kwa mara vinafaa vitundikwe kwenye stand maalumu mahali panapofikika kiurahisi mfano juu ya dressing table ili iwe rahisi kuvichukua na kutumia kila unapohitaji na kuzuia visishikane na hatimaye kuharibika.
 • Vito vya thamani viwekwe mahali salama kwenye container au box dogo zikizungushiwa kitambaa laini au sponji ili kuhifadhi thamani na mng’ao wake.
 • Hifadhi vitu vya aina moja pamoja, mfano dhahabu, silva, plastic, shanga, n.k ili iwe rahisi kujua kitu fulani kipo wapi kinapojitajika.
 • Hakikisha mikufu yote imefungwa vyema kuepuka kushikana na hatimaye kukatika.

Viatu

 • Viatu unavyovivaa mara kwa mara viweke kwenye ‘shoe rack’ mahali ambapo ni rahisi kuonekana kama ni kwenye korido au sehemu  yoyote rahisi kufikika.
 • Vipange viatu vyako kwenye shoe rack kufuatana na rangi, urefu wa kisigino, aina ya kiatu au matumizi.
 • Hakikisha viatu vyako ni vikavu na safi kabla ya kivihifadhi na hifadhi sehemu kavu isiyo na maji au unyevu.
 • Viatu ambavyo havivaliwi mara kwa mara kama vile vya kuvaa kwenye matukio maalinu ya usiku ni vyema vikihifadhiwa kwenye sehemu ya chini ya kabati.

Pochi

 • kama viatu pochi pia zinapendeza na pia kukusaidia kuokoa muda zikihifadhiwa kwa ukubwa, rangi, aina au matumizi.
 • Pochi unazotumia mara kwa mara weka kwenye stand maalumu na nyingine unaweza weka kabatini ili kupunguza wingi wa vitu kutundikwa kila mahali.
 • Pochi ndogo na wallet ziwekwe pamoja ndani ya droo au pochi kubwa ili kuepuka kupotelea ndani ya nguo au pochi nyingine.

Shalom

Dada Maria aliulizia kuhusu maternity wear ambazo zinaweza kuvaliwa ofisini na ukaonekana vizuri. Hapa kuna baadhi ya nguo ambazo zinafaa kuvaliwa ofisini kwa mtu ambaye hapaendelei kuvaa suruali. Kuna maternity sketi ambazo tumboni kunakuwa na belti kubwa la mpira la kukuwezesha kuvaa bila kupata tabu. Vile vile unaweza kuvaa magauni yenye mikono midogo mizuri au yasiyo na mikono na kisha kuvaa na koti dogo zuri au vijisweta vidogo na kukufanya ukaonekana mrembo na mwenye kupendeza.

Nadhani nitakuwa nimekusaidia, na wengine pia.

Ubarikiwe

Shalom

Muda mrefu hatujaongelea mambo ya urembo na mavazi na leo nimeonelea tuangalie kidogo mavazi mbalimbali yanayopendeza kuvaliwa wakati wa ujauzito. Wengi tumezoea kuvaa nguo kubwa za vitenge zinazofika hadi chini, ni sawa kabisa lakini inapendeza ukiwa unavaa nguo za aina tofauti tofauti ambazo ni nzuri na hazikubani wala kukufanya ukaonekana mkubwa sana.

Hapa kuna baadhi ya nguo ambazo ukizivaa wakati wa ujauzito kwa kweli zinavutia, unaweza ongezea nakshi kama skafu, mtandio au hata kikoti kidogo na wewe mwenyewe ukajisikia vizuri.

Maoni?  Ushauri?

organized-closet

Mara nyingi unaweza kukuta mtu ana kabati limejaa nguo hadi zinakosekana pa kuwekwea na katika hali halisi anajiona hana nguo za kuvaa. Hali  hii inatokana na kukosa mpangilio wa nguo kwenye kabati na pia kuweka nguo ambazo hazihitajiki tena. Nguo zisipokuwa na mpangilio maalumu ni ngumu sana kutafuta nguo gani uivae na ipi maana hujui ipo upande gani wa kabati. Pia pale unapohifadhi nguo ambazo unajua hutazivaa tena inasababisha kabati kujaa bila sababu. Njia hizi zitakusaidia katika kupanga kabati lako:

1. Tafuta siku ambayo unamuda wa kutosha na toa nguo zako zote kabatini kisha tenga zile ambazo unahitaji kuzivaa na zile ambazo unaona hutazivaa tena ( iwe zimekubana, zimechakaa, hauzitaki tena n.k).

2. Tafuta mfuko safi uweke nguo zote ambazo hutazivaa tena ambazo upo tayari kugawa kwa wenye uhitaji. Ni vyema ukianzia nyumbani mwako, kama una dada wa kazi unaweza mpa zile ambazo zitamfaa na kisha nyingine ukapelekea wengine wenye mahitaji unaowafahamu kama ni kanisani au mahali popote pale. Ila jihadhari usimpe mtu nguo iliyochakaa sana, haipendezi.

3. Nguo ambazo unazihitaji zitenge katika makundi (blauzi, sketi, magauni, n.k) na kisha uzikunje vizuri na kuzipanga kabatini kila kundi sehemu yake. Hii itakusaidia ukiwa unatafuta gauni unajua uangalie sehemu gani.  Nguo zinazoendana pamoja kama suti au vitenge ni vyema zikawekwa pamoja sketi na blauzi yake. Kama kabati lina nafasi kubwa makoti ya suti yakiwekwa kwenye henga yanapendeza zaidi.

4. Vitu kama mikanda, skafu, mitandio n.k viwekwe mahali pake ili iwe rahisi kupatikana pale vinapohitajika.

Jitahidi uwe na tabia ya kupanga nguo zako kila unapozifua. Ilikuepuka kutafuta nguo asubuhi na hatimaye kuharibu mpangilio wa kabati lako ni vyema kama utakuwa na utaratibu wa kunyoosha nguo za wiki zima kila mwisho wa wiki, hii itaokoa muda na ‘stress’ za kutafuta nguo ya kuvaa kila asubuhi.

Ubarikiwe.

ist2_8190319-women-s-shoes

Viatu ni kinga kwa ajili ya kuhifadhi miguu. Vile vile viatu ni vazi ambalo linaongeza urembo na nakshi kwa mvaaji. Viatu vipo vya aina mbalimbali na vinavaliwa kulingana na mahali na  mavazi yanayoambatana navyo. Tuangalie baadhi ya aina za viatu  na wapi hasa na vipi vikitumika vinapendeza zaidi.

1.Viatu vya ngozi vya kufunika

Viatu vya kufunika vipo virefu sana, vyenye urefu wa wastani na vifupi kabisa. Mara nyingine haviwi vya ngozi kabisa bali ni kama vina plastiki na pia vingine huwa na uwazi mdogo kwa mbele.Viatu virefu zaidi mara hupendeza zaidi kuvaliwa kwenye sherehe na kanisani. Unaweza kuvaa kazini kama kazi yako haikulazimu kutembea tembea maana vitachosha miguu yako na kupunguza ufanisi.

Viatu vyenye urefu wa wastani unaweza kuvaa popote iwe kazini, kanisani, kwenye sherehe n.k. Viatu vya chini kabisa vinakuwa vyenye matumizi zaidi wakati unamatembezi mengi. Havifai sana kuvaa kwenye sherehe za usiku hasa kama unavaa nguo maalumu ya usiku. Vinafaa sana kwa mjamzito hasa katika miezi ya mwisho.

2.Viatu vya wazi virefu

Viatu hivi vipo vya aina mbili, vyenye rangi za mng’ao na ambavyo ni mahususi kwa sherehe za usiku na vyenye rangi ngumu ambavyo waweza kuvaa kazini au kanisani. Viatu hivi vinapendeza kuvaliwa na nguo yoyote ila ikiwa ya urefu wa wastani ni nzuri zaidi maana huwezesha kuonekana urembo na uzuri wote wa kiatu. Viatu hivi vinakuja katika mitindo mbalimbali na unachagua ule ambao wewe unaupendelea zaidi mfano vyenye visigino vyembamba, visigino vinene au aina ya ‘wedges’.

3.Viatu vya wazi vifupi

Viatu hivi ni vizuri sababu vinawezesha miguu kupumua na ku’relax’. Viatu hivi vipo vya aina tofauti tofauti na vinafaa sana kuvaliwa kwa matembezi ya jioni, wakati wa safari ndefu, wakati ukiwa na mizunguko mingi na pia hata kazini au kanisani pale unapokuwa umevaa nguo za kawaida (casual). Havivutii sana kuvaliwa na suti au nguo ya usiku. Pia mara nyingi viatu vya chini hupendezea kuvaliwa na nguo ndefu( hasa casual) na viatu virefu hupendeza zaidi kwa nguo yenye urefu wa wastani.

4.Viatu vya muda maalumu

Hivi ni viatu ambavyo vinavaliwa wakati wa kazi maalumu kama wakati wa kazi za mashambani, mgodini, wakati wa michezo au wakati wa baridi kali.

 Ni vyema na inapendeza kama unauwezo uwe na viatu vya aina mbalimbali angalau aina tatu. Mfano viatu vyeusi vya urefu wa wastani, viatu vya usiku vya wazi, viatu vya chini vya kufunika na vya wazi.

scarfs

Skafu ni urembo unaoweza kuvaliwa na aina yoyote ya nguo iwe ni vazi la kawaida au suti ya aina yoyote. Skafu inawezesha nguo kuonekana ya kuvutia hata kama nguo ni ya kawaida kabisa. Skafu zipo za aina nyingi kama pashmina(mitandio), ndefu nyembamba, za mraba n.k.

Uvaaji wa Skafu

Skafu inaweza kuvaliwa katika mitindo mbalimbali kutokana na umbo lake na mvaaji anataka kuivaa vipi. Skafu inaweza kuvaliwa shingoni, kiunoni kama mkanda au kichwani kama kibanio au kufunika nywele. Skafu kubwa kama pashmina unaweza uitumia kujifunika hasa wakati wa baridi.

Ufungaji wa skafu shingoni

1.Skafu yenye umbo la mraba unaweza kuikunja kupata pembetatu kisha ukafunga pembe mbili nyuma ya shingo ili ule upande mpana uwe umelala kifuani chini ya shingo.
2.Skafu ndefu nyembamba inavaliwa kwa kuining’iniza shingoni na kuifunga na pini kwa mbele. Unaweza tumia ‘brooch’ au pete maalumu.
3.Skafu ndefu pia unaweza kuivaa shingoni upande mmoja ukining’inia kwa mbele na mwingine ukining’inia kwa nyuma.
4.Pashmina skafu unaweza kuivaa kwa kuikunja nusu na kuiweka shingoni kisha kuchukua upande mmoja na kuuweka ndani ya upande mwingine kama unafunga kamba.

Hadi wakati mwingine, Ukae na amani ya Bwana.

Next Page »

Follow

Get every new post delivered to your Inbox.

Join 152 other followers