Kuwa na Malengo

Malengo kwa maneno mengine unaweza kusema ni maono (vission/goals). Ni mambo ambayo unayatarajia baada ya kufanya kitu fulani kwa muda fulani.
Mithali 29:18 biblia inasema pasipo maono watu wanaangamia. Wewe kama mwanawake / msichana unayemjua Mungu ni lazima uwe na malengo na maisha yako. Ndiyo, tunajua kuwa Yesu anarudi lakini ni lazima uwe na malengo juu ya maisha haya maana hakuna ajuaye siku wala saa.
Bila kuwa na malengo hutajua kama umefikia mafanikio au la, hutajua kama uongeze bidii kiasi gani, utaona kuwa maisha ni safi tu kumbe sababu hauna malengo.

Kwa wale wanaojua mchezo wa ‘darts’, wachezaji wanakuwa makini kunakikisha mishale yao inafika kwenye target na hapo ndipo unakuwa umeshinda.Sasa bila hiyo target hutajua kama umepatia ama umekosea. Vivyo hivyo katika maisha lazima uwe na target ambayo unataka kuifikia. Kama ni kimasomo, biashara, huduma n.k.

Yakupasa uwe na malengo ya muda mfupi na yale ya muda mrefu. Ili malengo yawe sahihi ni lazima yawe malengo makini, yenye uhakika, ambayo yanatekelezeka na yawe ndani ya muda maalumu. Baada ya kuweka malengo yako mkabidhi Bwana na kumwomba akuwezeshe kuyatimiliza kwa mpango wake.Kisha hakikisha kila unalolifanya unaangalia malengo uliyoyaweka ili kuyatimiliza.
Mungu akusaidie unapotafakari haya na kukaa chini na kuweka malengo yako.

Mungu akubariki sana.

Advertisements

Malezi ya Mtoto

Nawasalimu wote katika jina la Yesu. Habari za weekend, nadhani wengi wetu tulikuwa katika nyumba ya Bwana kwa ibada mbalimbali.
Katika mada ya leo nitagusia zaidi kwa mtoto ambaye bado hajazaliwa.Watu wengi wanafikiri kuwa maisha ya mtu yanaanza pale anapozaliwa, lakini katika Yer 1:5 Mungu anamwambia Yeremia kuwa alimtakasa tangu tumboni mwa mama yake.Hivyo tunaona maisha ya mtu yanaazia tangu tumboni.Tena anasema ‘..kabla sijakuumba nalikujua..’ inaonyesha Mungu anamfahamu mwanadamu kabla hata ya kumuumba.
Pia katika Mwanzo 25:23 tunaona watoto wa Isaka walianza kushindana tangu tumboni. Hii ni mifano michache kuonyesha maisha yanaanza tangu tumboni.
Kutokana na kweli hii, malezi ya mtoto yanatakiwa yaanze tangu pale unapotarajia kupata mimba. Lazima ujiandae kiroho kwa malezi ya mtoto ambaye Bwana atapenda kukupatia.
Hapa nimeonyesha mambo machache unayoweza kufanya kama mama / mzazi:

 • Omba kwa ajili ya mtoto unayemtarajia (ombea uumbaji wake, ulinzi, na mapenzi ya Mungu kwa mtoto unayemtarajia)
 • Soma maneno ya Mungu kwa mtoto aliye tumboni.
 • Tamka maneno ya baraka, ushindi, upendo na amani kwa mtoto aliye tumboni
 • Mshirikishe baba wa mtoto katika malezi haya
 • Hakikisha nyumba ina furaha na amani mara zote maana huzuni ya mama inamadhara kwa mtoto aliye tumboni

Haya wapendwa kwa leo naishia hapa, Mungu azidi kutufundisha zaidi na zaidi.

Mungu akubariki sana.

Upangaji wa nyumba

arrange

Upangaji wa nyumba hasa sebule, jikoni na vyumbani ni jambo ambalo kila mwanamke anapenda alifanye kwa ukamilifu. Tatizo linakuja muda wa kufanya hivyo unakuwa hafifu sababu ya shughuli nyingi za ujenzi wa taifa na kazi ya Mungu pia.
Kuna njia nzuri ya kukuwezesha kufanya hivyo kwa muda huo kidogo ulio nao. Kwanza angalia zile sehemu ambazo zinahitaji muda mrefu ili ziwe nadhifu, kwa mfano jikoni, kabati languo, chumba cha watoto, shelfu la vitabu n.k.
Panga muda wa dakika 15 kila siku ambao utautumia kufanya shughuli hii. Anza na eneo moja kwanza hadi umalize ndio uende sehemu nyingine, ikiwezekana weka alarm ili usitumie zaidi ya dakika 15.
Mwanzo kazi itakuwa ngumu hasa kama hukuwa na utaratibu wa kupanga mara kwa mara ila baadaye utaona ilivyo rahisi kuweka nyumba yako nadhifu bila kutumia nguvu nyingi.
Inatosha kwa leo.

Mungu akubariki sana.

Mada: Mavazi ya heshima ni yapi?

shalom wapendwa

Leo naona tujadiliane kidogo kuhusu jambo ambalo limekuwa tata miongoni mwa wakristo waliookoka. Swala la mavazi limekuwa na tafsiri nyingi, sasa naomba tusaidiane kwa msaada wa Roho mtakatifu, yapi ni mavazi ya heshima yamfaayo mwanamke mtumishi wa Mungu? ambayo hayataharibu ushuhuda wake?.

Nakaribisha maoni mbalimbali ili tuweze kujifunza kwa pamoja.

Mungu akubariki sana

Kitchen Party

utensils

Shalom wapendwa
Baada ya mitandio kuchukua nafasi kubwa sana kwenye sherehe za ‘kitchen party’ baada ya khanga kumaliza muda wake, sasa nayo imeshapitwa na wakati.
Mtindo ulioingia sasa ni vitenge na vinapendeza haswa! Bibi harusi mtarajiwa anashona vazi lake maridadi la vitenge na wageni wote waalikwa wanapewa kitenge cha kushona rangi sawa na bibi arusi ila maua tofauti. Hakika inapendeza sana.
Kwa wale wanaotarajia kufanya sherehe hiyo tafuteni vitenge muone jinsi mtakavyo pendeza.
Next time nitawawekea picha mjionee wenyewe.
Kwa leo naishia hapa, wakati mwingine tena

Mungu akubariki sana.

Kumtumikia Mungu

Shalom
Leo tuangalie kuhusu kumtumikia Mungu sisi kama wanawake.Zipo kazi nyingi sana nyumbani mwa Bwana.Imezoeleka miongoni mwa wengi kwamba kuwa mtumishi wa Mungu ni lazima uwe na kati ya zile huduma tano au uwe muimbaji wa injili. Watu wengi wanasahau kuwa pamoja na hizo pia zipo kazi nyingi sana ndani ya nyumba ya Mungu ambazo tunaweza kuzifanya na kuwa watumishi wake.
Warumi 12:4-8
Sisi tu viungo katika mwili wa kristo. Tunafanya kazi kila mtu kwa kadiri ya mwito wake ila kwa kusaidiana na kwa umoja. Kama mwanamke wa kristo unaweza kuwa unawaangalia wajane na yatima (kama dorkasi), unafanya usafi wa kanisa kwa kujitolea, unawapa watoto wasio na wazazi uji jumapili baada ya shule ya jumapili, kuwatembelea na kuwatia moyo waliovunjika moyo, kuwafundisha stadi za maisha wenye uhitaji huo katika nyumba ya Bwana, kuangalia nyumba ya mtumishi wake mchungaji (mfano kupeleka maji kama ni tatizo, chakula,mavazi etc), na nyingine nyingi kutokana na eneo unapoishi.
Mungu atusaidie tunapoamua kumtumikia yeye kwa roho na kweli. Amua kutumika katika nyumba ya Bwana na hakika unaiona amani na furaha yake jinsi unavyoendelea kumuishia yeye na kumtumikia.

Mungu akubariki sana.

Bajeti

budget11

Nawasalimu wapendwa katika jina la Bwana, ni siku nyingi kidogo sikuwa hewani sababu ya matatizo kidogo ya kiafya..namshukuru Mungu kwa uponyaji wake na sasa tuendelee kujifunza katika uwepo wake.
Leo nimeona tuzungumze kuhusu bajeti.Hili jambo limekuwa ni gumu sana miongoni mwetu wanawake hasa kutokana na asili yetu ya kupenda kupendeza na kuwa na vitu vizuri.
Jambo muhimu ni kujua kiasi unachopata kwa mwezi ukitoa kodi zote, kiasi ambacho unatakiwa ukipangie matumizi.Kwa kawaida yapo matumizi ya aina kuu mbili, haijalishi unafamilia au unaishi mwenyewe na aina hizo ni matumizi ya lazima na matumizi ya ziada.
Matumizi ya lazima ni kwa mfano:

 • matoleo mbalimbali
 • Kodi ya nyumba
 • Ada za shule
 • Chakula
 • mahitaji ya nyumbani mf.sabuni,mafuta etc
 • Nauli / mafuta ya gari
 • Bili za umeme, maji,msaidizi,mlinzi n.k
 • Mawasiliano
 • Matibabu
 • Akiba

Mahitaji ya ziada ni kama

 • Nguo na viatu
 • Michango na zawadi
 • Burudani

Tenga kiasi kinachohitajia kwa kila kipengele kwa mwezi.Hakikisha fedha uliyotenga inatosha na usibadili matumizi ya fedha bila sababu ya msingi.
Fedha inayobaki kwa mwezi weka pembeni kama akiba au unaweza itumia kwa matumizi ya ziada.Marazote hakikisha umekamilisha matumizi yote ya lazima kabla ya kutumia kwa matumizi ya ziada.Na matumizi ya ziada yanaweza yakawa ni kila baada ya kipidi fulani mfano miezi 3, 6 n.k ili kuweka akiba zaidi kuliko kutumia fedha.

Hakikisha unaifuata bajeti yako kama ulivyojipangia ili uweze kuona mafanikio.Mwanzo itakuwa ngumu kidogo ila kadri unavyojizoeza baadaye itakuwa rahisi sana.

Epuka kununua kitu bila kukipangia bajeti..Tumia pesa yako kwa busara kwa mafanikio yako na familia yako.Pia jitahidi kuwafundisha watoto jinsi ya kutumia fedha kwa uangalifu na kwa bajeti.

Mungu akubariki unapochukua hatua hii muhimu katika mafanikio yako ya kifedha.