Ongea Habari Za Mungu Na Watoto Wako

children_field

Shalom

Je Mungu ni sehemu ya mazungumzo yako ya kila siku na watoto wako? Au unakwepa kuongea nao habari za Mungu? Watoto wako wanamuona Mungu katika maneno yako ya kila siku? Kitu unachokithanimi utawekeza muda wako, mali na hata nguvu zako. Watoto wako waone jinsi unavyowekeza kwa Mungu katika kulisoma neno lake, kuomba, kuhudhuria kanisani na kutumika katika kazi ya Mungu.

Tunapozungumza ukuu wa Mungu na watoto wetu katika maisha ya kila siku tunawajengea hazina kubwa ya imani kwa Mungu wao ambayo watakuwa nayo siku zote. Pamoja na kuwahamasisha kupata maksi nzuri darasani, kujihusisha na michezo na kufanya kazi za nyumbani hakikisha unawafundisha kumtumikia Mungu katika umri wowote walionao. Neno la Mungu liwe sehemu ya maisha yako na watoto wako siku zote.

KumbuKumbu 11:18-19 “Kwa hiyo yawekeni maneno yangu mioyoni mwenu na rohonu mwenu; yafungeni yawe dalili juu ya mikono yenu, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yenu. Nayo yafunzeni Vijana vyenu kwa kuyazungumza uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo

Advertisements

Kusamehewa Sio Kibali Cha Kuendelea Na Makosa

lady_sea

Kusamehewa hakukufanyi wewe uendelee na makosa eti sababu unajua kuwa utasamehewa. Unapoomba msamaha maanisha unachokisema na dhamiria kutoka moyoni kutokurudia tena kosa na epukana na mazingira yaliyokufanya ukatenda kosa hilo. Kuna watu kwa makusudi wanafanya makosa na kuyarudia wakijua kuwa wenzi wao watawasamehe sababu ni wepesi kusamehe. Unakuta mtu anafanya uzinzi, anasamehewa, anaendelea na wala hajali, au mtu anampiga mke wake, anasamehewa na anaendelea tena na tena.

Kusamehe hakumaanishi kuwa mtu upo tayari kuhatarisha maisha yako. Unaweza kumsamehe mtu anayekupiga lakini ukajitenga mbali naye sio sababu hujamsamehe bali kwa usalama wako watoto kama wapo na yeye pia maana anaweza kukudhuru akaishia gerezani, mpaka pale atakapoamua kweli kubadilika. Kusamehe hakumaanishi kuishi katika mateso.

Nawewe uliyesamehewa na kisha ukaendelea na makosa ukijua utasamehewa kumbuka ghadhabu wa Mungu ipo na hakika usipogeuka na kuiacha njia yako mbaya hauwezi kuiepuka!

Bible Study

loving_arms2

SOMO: HANA – UTHABITI KATIKA MAJARIBU

MAANDIKO: 1 SAMWELI 1:1-28; 2:1-10

Hana alikuwa ameolewa na mtu aitwaye Elikana. Elikana alikuwa na wake wawili wa kwanza akiitwa Penina na wa pili Hana. Penina alikuwa amejaliwa watoto wa kike kwa wa kiume lakini Hana yeye hakuwa na mtoto. Hali hiyo ilikuwa inamuumiza sana, mumewe alijitahidi kumuonyesha upendo na kujali ila bado moyo wake ulikuwa na mzigo mkubwa. Penina hakuwa msaada bali alizidisha maumivu ya Hana kwa kumchokoza kwa sababu ya kukosa mtoto.

Hali hiyo ya maumivu ya kukosa mtoto na kuchokozwa ilimpelekea Hana kuwa na maombi mazito mbele za Mungu. Hapa tunaona jinsi Hana alivyokuwa mwanamke thabiti wa imani, alikuwa na kila sababu ya kulalamika na kuona kama Mungu amemsahau au kuingia kwenye malumbano na Penina. Yeye alitambua kuwa mwenye uwezo wa kumpa mtoto ni Mungu na kamwe hawezi kushindwa, aliingia kwenye maombi na kukazana na maombi akiamini Mungu atafanya. Alimwekea Mungu nadhiri kuonyesha ni jinsi gani anahitaji mtoto.

Tunaona pia akiwa kwenye maombi mazito hadi sauti ikawa haitoki, kuhani Eli alidhania amelewa. Unaweza ukaona ni jinsi gani Hana alikuwa anaomba kwa uchungu, na alijisikiaje vibaya baada ya kuhani kuanza kumgombeza kuwa atalewa hadi lini wakati yupo kwenye majonzi mazito. Lakini majibu yake yanaonyesha kuwa Hana hakuruhusu maneno yale yamuondoe kwenye kusudi la maombi yale, hakuruhusu maneno yale ya kukatisha tamaa yaweke uchungu ndani yake bali aliendelea kuwa mnyenyekevu akimwamini Mungu. Unaweza kuwa unapitia magumu sana katika maisha halafu wale unaowategemea wakutie moyo na kukufariji ndio wakawa wa kwanza kukutuhumu na kukulaumu.

Tujifunze kwa Hana, usiyaweke moyoni maneno hayo wala usikubali yakutoe kwenye maombi yako kwa Mungu. Vile vile hapa tunaona shutuma za Eli hazikumfanya Hana amuone hafai na kutokumsikiliza. Aliendelea kumheshimu kama kuhani na alisikiliza neno lake na kulifanyia kazi. Wengi wetu hapa tungeshindwa. Tujifunze kwa mwanamke huyu mwenye imani thabiti. Endelea kumwamini Mungu, endelea kumimina moyo wako mbele za Mungu na hakika wakati utawadia na Bwana atatenda kwa utukufu wake. Wakati wa Bwana utawadia tu, Bwana mwenyewe atawanyamazisha wanaokushutumu na kukuchokoza kwa sababu ya hali uliyonayo. Usitafute wewe kuwanyamazisha, tujifunze kwa Hana alivyokabiliana na Penina bila kujibizana naye.

1 Samweli 1 : 20 – Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.

Pia tunaona kuwa Hana alikuwa mwaminifu kumtolea Mungu nadhiri aliyoiweka. Pamoja na kuwa alihitaji mtoto sana lakini hakuacha kumpeleka hekaluni kama alivyoahidi kwenye maombi. Unapokuwa katika maombi kama huna uhakika na uwezo wa kuitumiliza nadhiri ni vena usiiweke. Uwekapo nadhiri yako kwa Mungu hakikisha umeiondoa pale Mungu anapo kutendea.

Kumbukumbu la Torati 23 : 21 – Utakapoweka nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.

Mhubiri 5 : 4 – 5 Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri. Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe.

Tunamaliza somo letu kwa wimbo wa sifa kutoka kwa Hana. Hana alimwomba Mungu kwa machozi na alipotendewa alirudi na wimbo wa shukrani. Je umemshukuru Mungu kwa yale amekutendea au unaona ni sababu ya maombi yako mengi na mazito ndio maana umepata? Ukisoma sura ya pili hapo utaona shukrani zake kwa Mungu. Ameonyesha kabisa kuwa ni Mungu tu aliyetenda na mwenye nguvu, yeye hana la kujisifia. Tujifunze katika hili.

Maswali

1. Nini kilimpa Hana uchungu mwingi? Je ni maneno ya Penina.? Shutuma za Kuhani? Kutokuwa na mtoto?

2. Alikabiliana vipi na maumivu na uchungu ndani yake?

3. Unadhani ilikuwa rahisi kukabidhi mtoto kwa kuhani baada ya kumsubiri kiasi hicho?

4. Ni kiasi gani maneno ya watu ya kukatisha tamaa na kuvunja moyo yamekuathiri na kukuzuia kufikia ndoto zako?

5. Pale Unapokuwa na hitaji kubwa ila hauoni kama linapatikana huwa unakabiliana vipi na hali hiyo?

6. Je pale kiongozi wako wa imani anapokuonyesha kutokuamini unayoyafanya na kukushutumu huwa unakabiliana vipi? Je huwa unaendelea kumsikiliza akisema maneno ya Mungu?

7. Umejifunza nini kupitia maombi ya shukrani ya Hana?

Limeandaliwa na womenofchrist.wordpress.com

WANAWAKE WA BIBLIA

Shalom Leo tunanza somo letu la kwanza ambalo litakua ni mfululizo wa masomo juu ya wnawake wa biblia Tutaangalia maisha yao, familia zao, huduma na kazi zao, mafanikio yao, makosa yao na kushindwa kwao ili tuweze kujifunza kutoka kwao kwa msaada wa Roho mtakatifu.

SOMO LA KWANZA: DEBORA NA YAELI – UONGOZI THABITI NA USHUJAA

Wengi wetu tumewahi kumsikia Debora ila ni wachache wanaojua Yaeli ni nani. Tujifunze

KITABU: Waamuzi sura ya 4 na ya 5 ( Hakikisha umesoma zote)

Debora alikuwa ni nabii mke na kiongozi wa wana wa Israel ajulikanaye kama mwamuzi. Alikuwa ni mwamuzi mwanamke pekee. Debora pia alikuwa ameolewa na mtu aitwaye Lapidoti. Baada ya kifo cha Joshua aliyewaongoza wana wa Israeli kuingia kanaani, Mungu aliinua waamuzi kuwaongoza na kuwatawala. Waamuzi wa mwanzo walikuwa ni Othnieli, Ehudi na Shamgari. Debora alifuatia baada yao. Utayapata haya katika sura ya 3 ya kitabu cha waamuzi.

Wakati huo wa uongozi wa Debora, mfalme Yabini ndio alikuwa !tawala wa Kanaani na jemedari wake wa jeshi aliitwa Sisera. Wakaanani walikuwa na nguvu kubwa sana ya kijeshi na ndio walikuwa wanaongoza kwa kuwa na askari wengi na Vifaa Vya kisasa. Waliwatawala Israel kwa mabavu huku wakiwatesa kwa miaka 20. Debora alijikuta anasimama katika kipindi kigumu sana kwa taifa la Israel. Debora anatambulishwa kama nabii make kwanza Kabla ya muamuzi, hii ni sababu nafasi ya nabii alikuwa ni nafasi ya kipekee sana. Ni nabii pekee ndio alikuwa na uwezo wa kuongea na Mungu kwa niaba ya watu.

Mungu alimuahidi Musa kuinua manabii katika Israel na alipofanya hivyo hakuinua wanaume pekee bali na wanawake pia japo kipindi hicho wanawake hawakuwa na nafasi sana katika jamii.

KUM. 18:15‭, ‬18 BWANA, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye. Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.

Manabii wake wengine ni Miriam (Kutoka 15:20), Hulda (2wfalme 22:14), Noadia (Nehemiah 6:14) na mke wa Isaya (Isaya 8:2). Pamoja na kuwa mfumo wa maisha ulielemea kwa mwanume bado hikuwazuia wanawake kumtumikia Mungu.

Debora pamoja na kuwa nabii alikuwa ni mwamuzi katika Israel. Watu walikuwa wakimwende kupata suluhu ya matatizo yao mbalimbali.

Waamuzi 4:5 Naye alikaa chini ya mtende wa kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue.

Hii inaonyesha alikuwa na hekima ya kuweza kuwaamua, kibali na heshima katika jamii yake. Japokuwa biblia haisemi sana juu ya mumewe Ila inaonekana alikuwa anampa ushirikiano na hakuwa kikwazo cha mkewe kufanya kazi kwa ufanisi. Ndoa haipaswi kuwa kizuizi kwa mwanamke kutimiza ndoto zake na kumtumikia Mungu kwa karama na vipawa alivyopewa.

Ukombozi wa Israel kutoka kwa wa Kanaani ulianza pale Debora alipomuita Baraka na kumpa ujumbe wa kinabii kutoka kwa Mungu na kumwambia aandae jeshi la watu 10000 na kuwa Sisera anakuja kuwavamia ila wao wajiandae maana watamshinda sababu Mungu yupo upande wao. Kutokana na ukweli kwamba jeshi la Sisera lina vikosi vikali na zana za kisasa na wana wa Israel waliambiwa wachukue tu watu kutoka makabila fulani, Baraka alipata hofu akijua hawataweza kupigana na Sisera. Kutokana na hofu akahitaji uwepowa Debora ambaye Mungu amezungumza naye waende wote vitani. Baraka aliujua ujasiri wa Debora na kwamba uwepo wake ungewapa wanajeshi wake na yeye ujasiri wakijua Mungu yupo pamoja naye.

Waamuzi 4:8 Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi.

Pamoja na kufahamu kuwa Baraka amekubali kwenda vitani wa sababu yake, Debora hakupata kiburi wala majivuno kujiona kuwa yeye ni bora zaidi na yeye ndio kafanikisha. Alijua kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu tu na Mungu ndiye anayewapigania watu wake. Hakubeba utukufu wa Mungu wala kujionyesha kuwa yeye ni wa maana sana. Tabia hii ya kiungu ndio huwainua watu, tabia ya kujishusha na kuacha utukufu umwendee Mungu peke yake. Unapotambua kuwa unayoyafanya sio wewe wala kwa nguvu zako bali ni Mungu mwenyewe ndipo Mungu atazidi kukutumia zaidi na zaidi. Kusudi lake hikuwa kujipatia sifa Bali Mungu mwenyewe kujitwalia utukufu. Waamuzi 4:24

Hapa tunakutana na mwanamke mwingine shujaa aitwaye Yaeli. Waamuzi 4: 17-24

Yaeli alikuwa ni mkebwa Heberi, Mkeni Heberi na mfalme Yabini walikuwa na uelewano hivyo Sisera akaona akajifiche huko. Yaeli yenye akakumbuka asili yake ni Israel hivyo akaazimia kumuua Sisera mtesaji wa Israeli. Kwa ujasiri kabisa akamuua na kusababisha ushindi kwa Israel na unabii ukatimi kuwa Sisera atauwawa katika mikono ya mwanamke. Yaeli alikuwa tayri kupambna kwa ajili ya taifa lake maana aliijua historia yake na hakuwa tayari kuridhika na amani ya muda. Fursa ilipopatikana hakutana hofu kumuingia kumharibia kusudi lake bali aliitumia vizuri. Ni ujasiri wa kipekee ukizingatia mfalme ambaye ndio mkuu wa Sisera alikuwa na mkataba wa amani na mumewe.

Utawala wa Debora ulipelekea kuwa na Amani kwa miaka 40, waamuzi 5:31. Kizazi chote kiliishi kwa amani kwa sababu ya wanawake hawa waliosimama katika nafasi zao kwa uaminifu. Sasa ni zamu yako kusimama kwa uaminifu pale Mungu amekuweka kwa manufaa ya vizazi vyote. Haijalishi ni ofisi, biashara, huduma, familia, jamii n.k. Simama kwa uaminifu katika nafasi yako na kamwe usitafute utukufu na sifa.

MASWALI

Maswali ya kuyajibu wakati unasoma somo hili kisha tutajadili pamoja siku ya Ijumaa. Hakikisha Leo hdi alhamisi umepata muda wa kuyajibu yote.

Soma Waamuzi 4 na 5 kisha andika majibu ya maswali haya kwenye daftari lako.

1. Nini kilimpa Debora nguvu ya kufanya kazi yake?

2. Tunawezaje kuwa na ufanisi kama wanawake watumishi wa Mungu katika kizazi hiki?

3. Yael ni nani?

4. Je unawezaje kulinganisha alichofanya Yaeli katika maisha ya Sasa?

5. Kuwa umuhimu gani kuwa na moyo safi?

6. Taja vitu vinavyoweza kuwasaidia wanawake kufanikisha kusudi la Mungu katika maisha yao na utumishi wao.

7. Jambo gani umejifunza binafsi kutokana na maisha ya Debora na Yaeli ambalo utalifanyia kazi kubadili maisha yako?

8. Unadhani ni gharama gani Debora na Yaeli walikubali kuingia ili kufanikisha kusudi la Mungu katika maisha yao?

9. Muelezee Debora katika maeneo yafuatayo

I. Wito wake

II. Utayari

III. Ujasiri

IV. Imani kwa Mungu

Ubarikiwe Sana unapojifunza somo hili kwa makini. Tukutane Ijumaa kwenye majadiliano

Limeandaliwa na: Magreth Riwa

womenofchrist.wordpress.com

Masomo ya Biblia ( Bible Study)

Shalom

Napenda kuwatangazia Kuanza kwa mfululizo wa masomo ya biblia (bible study ) mahali hapa. Masomo haya sio mahubiri hivyo kila anayetamani kulijua neno la Mungu kwa undani itamlazimu kusoma somo kwa makini na kusoma sehemu husika kwenye biblia yake na kisha kujibu maswali yatakayokuwepo. Kisha siku ya ijumaa itakuwa ni maalumu kwa majadiliano na maswali.

Somo litakuwa linawekwa kila siku ya jumatatu. Nakukaribisha sana tujifunze biblia pamoja. Unapaswa kuwa na biblia, daftari au notebook na kalamu. Kisha tenga siku na muda maalumu kila wiki wa kukaa na kusoma na kujifunza huku ukiandika kwenye daftari unayojifunza.

Tutaanza na mfululizo wa masomo juu ya wanawake wa Biblia. Maisha yao, utumishi wao, makosa yao, ushindi wao na tuna nini la kujifunza kwao. Kaa mkao wa kujifunza na kujadili.

Tutaanza rasmi tarehe 24 July.

Karibu sana

Mambo Muhimu Kwako

1. Kila unapoamka kutana na Mungu kwanza kabla ya kukutana na mtu yeyote. Anza siku yako kwa maombi na kuongea na baba yako.

2. Soma neno la Mungu kila siku. Tafuta bible study ya binafsi au kikundi kwa ajili ya kujifunza neno la Mungu.

3. Andika baraka zote Mungu anazokutendea kila wakati bila kusahau majibu ya maombi yako.
Hii itakupa kuwa na moyo wa shukrani na kukuongezea imani.

4. Tafuta mstari wa biblia wa kusimamia kwa wiki husika au mwezi au mwaka. Hakikisha kila siku unatembea na neno la Mungu linalokuongoza kutenda na kuwaza.

Ubarikiwe sana

JINSI YA KUWEKA MIPANGO YA MWAKA

Ufuatao ni mtiririko wa maswali ambayo yatakusaidia kuangalia na kukagua maisha yako na kupanga mipango yako kwa ajili ya mwaka huu. Jibu maswali haya kwa uhakika huku ukifikiria jinsi ya kuboresha maisha yako.

A: MALENGO BINAFSI
1. Ni Tabia gani nzuri ambazo kujijengea mwaka huu na hatua gani unapanga kuzichukua kufanikisha hilo?
2. Utafanya nini kuhakikisha kuwa unasimamia malengo yako bila kusukumwa?
3. Unapanga kujifunza kitu gani kipya mwaka huu?
4. Vitabu gani unapanga kuvisoma mwaka huu?
5. Je unaifurahia kazi yako? Ni nini kimakufurahisha zaidi au kinakukera zaidi kwenye kazi yako?

B: AFYA NA MUONEKANO
1. Ni jambo gani unataka kulifanikisha mwaka huu katika kutunza na kuboresha afya yako?
2. Utafanya mambo gani kila siku ili kuweza kufikia malengo yako ya afya.
3. Unapanga kufanya nini mwezi huu kufikia malengo yako ya afya ya mwaka?

C: NDOA NA FAMILIA
1. Muda wako na familia mwaka huu unapanga uweje?
2. Utafanya nini ili kuongeza ukaribu na mwenzi wako mwaka huu?
3. Ni mipango gani mliyonayo kama wanandoa kuimarisha ndoa yenu?
4. Mwaka huu mnategemea kwenda safari ya mapumziko? Mtaiandaa vipi?

D: WATOTO
1. Ni kwa namna gani unataka watoto wako wakue katika maeneo yafuatayo:
i. Kimwili
ii. Kihisia (emotionally)
iii. Kimahusiano
iv. Kiroho
v. Kielimu
2. Ni kwa namna gani watoto wako watasoma mwaka huu?
3. Uwezo wa watoto wako upo kwenye maeneo gani? Utawasaidie kuutumia vyema?
4. Udhaifu wa watoto wako upo wapi? Utawasaidiaje kukabiliana nao?

E: KIUCHUMI
1. Ni maendeleo gani unataka kuyaona mwaka huu katika uchumi wako?
2. Kipato chako cha sasa kikoje? Unawezaje kukiongeza?
3. Una madeni kiasi gani? Unawezaje kuyapunguza au kumaliza kabisa kwa mwaka huu?
4. Akauti yako ya akiba ikoje? Unawezaje kuweka akiba zaidi kwa mwaka huu?
5. Malengo yako ya kiuchumi ya muda mrefu ni yapi? Mwaka huu utafanya nini kuanza kuyatimiliza?
6. Je huwa unatoa sadaka na zaka zote? Kama la mwaka huu unaanzimia kutoa kwa kiwango gani?
7. Mwezi huu tunaanza kufanya mambo gani katika safari ya kuboresha uchumi wako?