Sifa za Mume Mwema

Shalom,

Siku zilizopita tulijifunza sifa za mke mwema na kutokana na maoni ya baadhi ya watu leo tuangalie biblia inasema nini kuhusu mume mwema.

1. Awe mwenye kumcha Mungu

Mume mwema ni yule anayeheshimu nafasi ya Mungu katika maisha yake, anayemcha Mungu na kuepukana na uovu wa kila aina. Anatambua kwamba Mungu ndiye anayepaswa kuongoza maisha yake na si vinginevyo.

Kumbukumbu 6:5 Nawe mpende BWANA Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.

2. Mwenye kumpenda mke wake kama nafsi yake

Kumpenda mke wake zaidi ya kitu chochote iwe ni wazazi, kazi, biashara, watoto n.k. Mume mwema siku zote huthamini nafasi ya mke katika maisha yake na mara zote mke wake ni namba moja kwake.

Mwanzo 2:24 Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

Efeso 5: 25,28 Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake,..vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye  mkewe hujipenda mwenyewe.

3. Mwenye uwezo wa kuiongoza familia yake

Inashangaza kuona baadhi ya waume hawawezi kusimama kama viongozi katika nyumba zao. Wanasahau kama Mungu kawaweka kama viongozi wa familia na mke ni msaidizi wake. Utakuta wengine wanaaacha jukumu hilo kwa mkewe kwa kupenda au kwa kutokupenda na wengine wanajikuta wamewafanya wazazi wao au ndugu zao wengine kusimama kama viongozi wa familia.Biblia inaweka wazi kuwa mume ni kichwa cha ndoa, ni lazima kila mume atambue hilo na ahakikishe anasimama kwenye nafasi  yake kwa uaminifu bila kujali hali  yake, wadhifa, kipato, huduma au chochote kile.

Efeso 5:23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe; kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.

4. Mwenye Kuihudumia Familia Yake

Mume mwema lazima ahakikishe anafanya kazi na kuipatia familia yake mahitaji ya kila siku. Haijalishi mkewe anafanya kazi au la, yeye kama mume anajukumu la kuihudumia familia yake na hii ni sehemu ya uongozi wake. Hapa pia inajumuisha na kuilinda familia yake juu ya hatari zote na kuhakikisha wana furaha na amani ya kudumu. Ili mke na watoto waweze kuwa na amani ni lazima wahakikishiwe usalama wao kimwili, kiroho na kiuchumi.

1Timotheo 5:8 Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.

5. Mwenye kuwafundisha watoto njia inayopasa

Mume kama kiongozi wa familia anajukumu la kuwafundisha watoto njia inayofaa akisaidiana na mke wake. Waume wengi wanafikiri kazi ya kuwafundisha watoto ni ya mama wao ni kutoa tu adhabu pale wanapoona mtoto amekosea lakini hawajishughulishi katika kuwafundisha. Mume mwema lazima alitambue jukumu lake la kuwafundisha watoto neno la Mungu na misingi ya maisha ya mkristo.

Kumbu kumbu 6: 6-7 Na maneno haya ninayokuamuru leo,yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena, uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.

Efeso 6:4 Nanyi wakina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya BWANA.

6. Mwenye kumheshimu mke wake

Imezoeleka kuwa mke ndiye anayepaswa kimheshimu mume, lakini biblia inawataka pia waume kuwahepa heshima wake zao na kuishi nao kwa akili. Haipaswi mume kufanya maamuzi yoyote yanayohusu familia bila kumshirikisha mke wake, yawe madogo kama lini mgeni fulani aje hadi makubwa kama ujenzi au kuanzisha biashara. Mke ni sehemu ya mume hivyo ni lazima mume ampe heshima yake na kuthamini mawazo yake na mchango wake hata kama mke hafanyi kazi ya kuingiza kipato. Kumbuka mke anabeba jina la mume wake na ni sehemu ya mume wake, inahuzunisha kuona waume wengine wakiwadharau wake zao mbele ya ndugu zao au marafiki. Haipasi kabisa kumgombeza au kumsema vibaya mke wako mbele za watu, iwe ni ndugu, watoto au mwingine yeyote.

1Petro 3:7 Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.

20 thoughts on “Sifa za Mume Mwema

  1. Bwana Yesu asifiwe,
    Nafurahi kwa somo zuri, namuomba Mungu anipe mume wa jinsi hii.
    Naamini atatenda kwa utukufu wake.
    Ubarikiwe kwa somo zuri.

  2. Shalom, nimebarikiwa sana na makala hii ninamuomba Mungu anionyeshe mwanaume mwenye sifa hizo pia atakayependezwa naye kwani yeye ndiye mpaji

  3. nashukuri kwa somo zuri kwetu wa dada,sababu mafunzo mengi kuhusu ndoa maranyingi uhusu wanawake tu!!!utazani wanaume huwa hayawahusu!!
    Mungu akubariki sana kwa kutuelimisha kinadada kuhusu waume wema.

  4. utamjuaje kuwa ana uwezo wa kufundisha familia, kuhudumia familia, kuheshimu mke wake wakati mnakuwa hamjaoana?

  5. Swali zuri, kama ambavyo sifa za mke mwema katika mithali 31 zilivyo huwezi kumtambua kabla hujamuoa. Biblia haina sifa za mchumba mwema bali sifa za kijana mcha Mungu. Unapaswa kumcha Mungu na kumwishia yeye naye atakupa kujana anayemcha na hatimaye mtafanyika mke na mume mwema. Ubarikiwe

  6. oh…nimefurahia sana hili somo japo nimechelewa kuisoma ila bado ninanafasi coz sijachagua mume mwema now nimefurahi zaidi baada ya kusoma sifa za mume mwema MUNGU akubariki mtumishi kwa kuelimisha jamii!! naamini Mungu atanipa mume mwema!!

  7. Asant kwa solo zuri
    Me nampenda mume wangu lakini naona ndoa yetu haina a man I mpka wakat mwingine najuta kuolew he nifanyeje ili kirudisha a man I ya zaman pamoja Na furaha? Sababu hatuongei kwa kucheka mpka wawepo wageni sasa inakua inaumiza moto wangu sana halo hii

  8. BWANA YESU ASIWE SANA.Nafurahi kwa somo zuri sana lakini migogoro iliyo mingi katika ndoa ni swala la uchumi ,inapotokea mume akafilisika mke ni rahisi kumwacha umewe kwa kujihusisaha na ngono nje ya ndoa ananza kuisaliti ndoa’pia inapotokea mume kapata pesa huwa baadhi anahamua kuingia nyumba ndogo .je tatizo ni lipi na utamsaidiaje?

Leave a comment