Achilia Na Songa Mbele

Mambo ya nyuma yasikufanye ushindwe kuifurahia leo yako au kupanga mipango kwa ajili ya kesho yako. Hakuna ambaye hajawahi kuumizwa iwe ni maisha/ mtu / watu au hali. Kinachotofautisha ni uamuzi wa kuachilia maumivu na machungu ya nyuma na kusonga mbele. Kuendelea kuyashikilia na kuyabeba kama bango haiondoi uhalisia kuwa yametokea wala hakufanyi leo yako kuwa nzuri.

Tambua kuwa maisha yako ni jukumu lako na si mwingine yeyote. Haijalishi umeumizwa vipi, unawajibika kuishi maisha yako kwa furaha na kufanya bidii ili kesho iwe bora zaidi. Aliyekukosea au kukusababishia maumivu hawajibiki kukupa furaha wala kukuondolea maumivu, ni jukumu lako asilimia mia. Amka sasa, jikung’ute maumivu yote na uchungu wa yaliyopita na usonge mbele.

Si kwa uweza wala nguvu zetu bali kwa msaada wa Mungu.

Advertisements

Malengo Ya Mwaka

Unapoanza Mwaka ni wakati muafaka wa kuweka malengo unayotaka kufanikisha katika Mwaka husika na mikakati ya utekelezaji. Bila kuweka malengo unawezakuta mwaka unaisha na hakuna kitu umekamilisha.

Nimeweka mtiririko wa maswali yatakayokusaidia kukuongoza jinsi ya kuweka malengo katika maeneo mbalimbali ya maisha kama kiroho, kiuchumi, afya, familia n.k

Download Malengo Ya Mwaka

Jinsi Ya Kufanya Maono Yako Yawe Hai

cropped-wpid-gardenofgrace.jpg

Bila ya kuwa na maono ya wapi unaelekea ni rahisi kuchukuliwa na upepo na kupelekwa usikokutazamia. Maono yatakufanya ujue ni nini ufanye kwa ajili ya Mungu na maisha yako kwa ujumla.

Mithali 29: 18 

Maono yako kwa ajili ya kazi ya Mungu ni lazima yaendane na agizo kuu alilolitoa Bwana Yesu kwa wote wanaomwamini.

Marko 16:15
 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe.

Ni lazima mara zote agizo hili liwe ndani yako ili unapoendelea na maono yako usijeenda mbali na agizo hili.

Shetani hujaribu kuyafisha maono yako na usipokuwa mwangalifu atayapoteza kabisa. Yeye mara zote hutaka kituzuia kuyafanya mapenzi ya Mungu, anajua akiyaua maono yetu hatutaweza kuifanya kazi ya Mungu kwa ukamilifu.

2Korintho 2:11 Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.

Mambo yafuatayo shetani huyatumia kuua maono yetu:

1. Dhambi ambazo hazijatubiwa
Isaya 59:9-12 Mistari hii inaonyesha kuwa dhambi isipotubiwa hupofusha macho ya rohoni hivyo hutaweza kuyaona maono yako. Dhambi inakuweka mbali na utukufu wa Mungu.

2. Uhusiano uliovinjika katika mwili wa Kristo 
Tunaporuhusu makosa ya ndugu zetu katika Kristo kuzaa uchungu badala ya kusamehe, tunaruhusu shetani kuyafunga macho yetu ya kiroho na hivyo kushindwa kuiona njia ya kuelekea kwenye maono yetu.

3. Tamaa ya mambo yanayoonekana

Zaburi 119:37 Unigeuze macho yangu nisitazame yasiyofaa, unihuishe katika njia yako.

Ukiangalia sana mambo ya dunia na tamaa zake utajikuta unayasahau maono yako na kubaki umefungwa na mambo hayo.

4. Kuangalia sana mambo ya nyuma.
Unapoacha kutazama mbele unapoelekea na kuweka nguvu na akili yako yote katika mambo ya nyuma yaliyopita, utapoteza kusudi lako na maono yako.

Mwanzo 19:26 Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.

Wafilipi 3:13 Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele.

5. Kutumia muda mwingi kuangalia matatizo 
Shetani hujaribu kutufanya tuangalie tu matatizo tuliyonayo na yale yanayoweza kutokea tunapoyafanyia kazi maono yetu hivyo kutuondolea imani ya kuyakamilisha. Biblia katika kitabu cha hesabu inaelezea habari za wapelelezi kumi waliorudi na habari za kukatisha tamaa katika kuiendea nchi ya ahadi maana waliangalia zaidi matatizo na kupoteza maono yao ya kuingia nchi ya ahadi.

Joshua na Kaleb waliona zaidi ya matatizo, waliuona ukuu na uaminifu wa Mungu. Hawakuwa na hofu yoyote hivyo waliweza kuingia nchi ya ahadi (kukamilisha maono yao) maana walimwamini Mungu. Petro alijaribu kutembea juu ya maji lakini alipoona mawimbi akasahau Yesu aliyekuwa mbele yake akimwambia njoo, akaweka akili kwenye mawimbi akaanza kuzama.

Ili tuweze kuyafanikisha maono yetu ni lazima tuwe na uhusiano na ushirika wa karibu na Roho Mtakatifu.

Ubarikiwe na BWANA Yesu.

Usikubali Kufungwa na Yaliyopita

2911121736_15728ac5f0

Unapoamua kumfuata na kumuishia Mungu, maisha yako ya zamani hayawezi kukuharibia wala kuwa ndio dira ya maisha yako ya sasa na baadaye. Usikate tamaa kuwa hutaweza kufanikiwa maana wewe umezaliwa katika shida, umetenda maovu sana au ukadhani umekuja duniani kwa bahati mbaya. Kila mmoja amezaliwa kwa kusudi la Mungu. Mungu anampango kamili wa maisha yako iwe umezaliwa mtoto wa nje, umezaliwa mimba ya utotoni, umezaliwa baada ya mzazi wako kubakwa, n.k. upo kwa kusudi la Mungu.

Sulemani alizaliwa baada ya Daudi kumchukua mke wa uria na kumuua uria hakini hiyo haikuondoa mpango wa Mungu juu ya sulemani. Peres alizaliwa baada ya tamari kujifanya kahaba na kulala na mkwe wake, lakini haikuzuia uzao wa Peres kuja kuwa uzao wa Bwana Yesu. Rahabu alikuwa kahaba, pale alipoamua kuungana na watu wa Mungu, kizazi cha Yesu kilipitia na kwake pia.

Usiangalie past yako, mwangalie Mungu na neno lake na uaminifu wake. Tafuta kulijua kusudi la Mungu katika maisha yako na uliishi. Yesu atabadili past yako ngumu kuwa kesho yenye ushindi na furaha.

Acha Kujihurumia Na Kulalamika

Kuna mtu aliniandikia message analalamika kuwa maisha yake yamekuwa ni ya mateso matupu, amekuwa mtu wa kuhangaika kwenye nyumba za watu mara leo anaishi na huyu mara na yule na anaona kuwa amezaliwa ili apate shida. Nilimtia moyo na kumpa maneno ya kumsaidia. Ila nimeona leo niliongelee jambo hili hapa.

Watu wengi sana wanasumbuliwa na hali ya kukosa shukurani. Ukimwambia mtu hivyo anaruka hapana mimi nashukuru kwa kila ninalopewa, ila ukweli unabaki kuwa tatizo hili linasumbua wengi. Na linaongezewa na hali ya kuona kuwa mtu mwingine ndiye anajukumu la kukupa furaha na kufanikisha maisha yako mfano mzazi, ndugu, rafiki, mume, mke n.n.

Nilikutana na mtu aliyenifundisha jambo kubwa sana kutokana na maisha yake,. Niliposikia habari za maisha yake nilijua nikikutana naye atakuwa mtu mwenye kusononeka, huzuni, anayejiurumia na kulaumu wengine lakini haikuwa hivyo. Alikuwa mtu aliyejaa furaha, mkarimu, anayepambana kuyakomboa maisha yake bila kuangalia changamoto lukuki zilizomzunguka na anayewajali na kuwasema vizuri wale ambao kwa uhakika walistahili kumsaidia lakini walimtenga.

Nikajifunza kuwa hata ukijihurumia na kulaumu mazingira yaliyopelekea hali yako kuwa hivyo kamwe huwezi kuibadili, unapaswa kumshukuru Mungu kwa vile ulivyonavyo na kuweka bidii, narudia bidii ili kuyakomboa maisha yako. Usiishie kuota, bali fanya kazi kwa uwezo wako wote. Mshukuru Mungu una watu wanaoweza kukupa mahali pa kulala hata kama ni wiki moja, mshukuru Mungu unapata chakula kuna ambao hata hizo nyumba za kuzunguka leo kwa huyu kesho kwa huyu hawana. Changamoto zako ziwe daraja la kukuvusha kuelekea mafanikio na sio utelezi kukupeleka shimoni.

Wewe Ni Wa Thamani

932402163-mother-holding-a-baby-with-head-on-shoulder
Pongezi nyingi kwako msichana uliyepewa mimba na kutelekezwa lakini hukuitoa bali uliamua kuilea na kuendelea kumlea mtoto wako peke yako bila hata ya msaada wa baba wa mtoto. Wamama wengi ambao hulea mtoto au watoto bila kuolewa maranyingi huonekana kama hawapo sawa kulingana na mfumo wa jamii. Jamii imekuwa ikiwa judge bila kujua nini wamepitia na wanapitia. Ni ukweli usiopingika kuwa watoto wanapaswa kulelewa na wazazi wawili lakini hii siyo sababu ya kumdharau msichana anayalea mtoto mwenyewe maana hujui nini kimepelekea hali hiyo.

Mungu awabariki sana na awakumbuke pamoja na watoto wenu. Usikate tamaa wala kujenga chuki na kisasi na baba wa mtoto, wewe endelea kuangalia maisha ya mtoto wako na kuboresha maisha yako na hakika Mungu hatakuacha na atakupa haja za moyo wako. Sisi wenye ndugu na marafiki ambao ni single mothers tujue wanatuhitaji kuwakubali, kuwatia moyo na kutowajudge.  Kama hajaamua kukuambia baba wa mtoto heshimu maamuzi yake na sio kila saa kumsumbua kwa maswali.

Thamani Ya Mwanamke

Mungu aliona si vyema adamu aishi peke yake akaamua kumtafutia msaidizi wa kufanana naye. Wanawake tumeumbwa kwa kusudi kamili la Mungu na tunajukumu la kuwa wasaidizi. Nafasi ya mwanamke katika jamii, familia, ndoa, kanisa na taifa ni kubwa sana. Angalia jinsi wanawake wanavyohangaika na watoto, kuanzia wakiwa tumboni hadi wakiwa watu wazima. Mwanamke ni mjenzi wa familia, mwanamke ni muunganishi wa familia na mwanamke ni mrutubishaji wa familia.

Moyo wa mwanamke unauwezo mkubwa sana, yani hawa nakaa nafikiria moyo wa mwanamke nashindwa kuuelewa kabisa, wanawake wanatendwa kila siku lakini wanasamehe, wanajitahidi kuachilia japo ni ngumu na wanaamua kuendelea kutenda mema. Unakuta mama anagundua mumewe anatembea nje, na hata anafikia kulala nje, mama huyu atalia, ataumia lakini atampikia chakula, atamfulia, atamuombea ataamua kumsamehe na hata akiletewa mtoto wa nje anamtunza. Hivi ni wanaume wangapi wanaoweza kuwasamehe wake zao wanaotembea nje? Na pale anaporudia na kurudia na wakati mwingine kulala nje???

Mungu awakumbuke wanawake wote.
Mungu asikie kilio chako unacholia ndani ya shuka na bafuni.
Mungu akuonekanie na kukurejeshea furaha ya maisha.
Mungu akutetee wewe ukiyepewa mimba na kuachwa.
Mungu akutunze wewe uliyetelekezwa na mume na ukaachiwa watoto.
Mungu awe mume wa wajane wote.
Mungu ailainishe mioyo ya waume wote, waitambue thamani ya wake walionao, Mungu awafunike macho yao wasione wengine zaidi ya wake zao.

Mungu alituumba kwa kusudi, tufurahie uanamke wetu na kamwe tusikubali changamoto za maisha zituondolee furaha. Mungu aliona dunia haitakuwa njema bila sisi ndio maana akaamua kutuumba, sisi ni wa thamani saanaaa….