Maandalizi ya Fungate

Baada ya kutoa orodha ya vitu vya kuhakikisha unakuwanavyo unavyoenda kwenye fungate (honeymoon), nimegundua kuwa maharusi wengi hawaelewi ni muda gani wa kujiandaa na kuandaa mahali pa kwenda kwa ajili ya fungate. Fungate ni kitu muhimu sana kwa ajili ya watu wanaooana hivyo ni lazima jambo hili lipewe kipaumbele linachostahili.

Pale mnapoanza mipango ya harusi ndio wakati muafaka wa kuanza kupanga kuhusu jambo hili. Ni muhimu kila mmoja wenu akawa huru kusema anataka mahali pa aina gani na mkubaliane kwa pamoja kwa kuzingatia vigezo mbalimbali. Kuna wakaka wengine wanapenda kuwafanyia wenzi wao surprise, hata kama ni surprise ni vizuri ukajua anapendelea nini usije ukamvunja moyo siku us kwanza ya ndoa yenu.

Mambo muhimu ya kuzingatia ni pamoja na:

1. Gharama ziwe zinalingana na uwezo wenu.
Hapa ni lazima utambue kuwa jambo hili ni la mara moja hivyo ni bora uwe na harusi ya kawaida ili muweze kupata hela nzuri ya kwenda mahali pazuri kwa ajili ya fungate.

2. Eneo lililotulia mbali na maeneo mnayoishi
Haitakuwa vyema kuamka asubuhi kwenda kupata kifungua kinywa siku ya kwanza ya ndoa yenu na kukutana na mama mkwe. Tafuta mahali patulivu, pembezoni mwa mji mbali na mahali mnapoishi. Kama mnampango wa kwenda mji mwingine msisafiri mara baada ya harusi, mpunzike kwanza angalau siku mbili ndipo msafiri.

3. Msitumie simu zenu angalau kwa wiki ya kwanza ili mpate muda wa kuwa na faragha ya kutosha. Unaweza kuwasha simu ukakutana na mambo ya kikazi au kijamii yakakuondolea furaha au concentration. Fungate no kwa ajili yenu kuwa wawili pamoja na kufahamiana kwa undani. Inashangaza sana kuona mtu anafunga ndoa jumapili halafu jumatatu unamkuta online facebook. Unapata wapi huo muda? Na kwanini? Fungate ni jambo la kulidhamini sana, ni muda wa kumpa mwenzi wako muda wako wote na usikivu wako wote na ukaribu wote. Ukiwa honeymoon inakubidi akili yako yote ijae mwenzi wako na maisha mnayoyaendea, achana na simu utaikuta tu baada ya kuweka msingi imara wa ndoa yako.

Kuna watu wanahoji umuhimu wa kwenda hotelini kwa ajili ya fungate. Mwili wa binadamu unahitaji kula, kukaa mahali safi na kuvaa nguo safi. Sasa mkienda nyumbani itabidi muwe na muda wa kupika, kufua na kufanya usafi, mambo haya yanawapunguzia muda wa kuwa intimate pamoja ukizingatia ndio mara ya kwanza. Hivyo ni vyema mkawa hotelini ili mpate muda mzuri wa kuwa pamoja.

Debora

Bible Study

Somo: Waamuzi 4

Katika kitabu cha waamuzi sura ya 4 tunaona maisha ya Debora. Debora alikuwa ni mwanamke mwenye vipaji mbalimbali na alivitumia vipawa vyake kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kuwasaidia watu wake. Alikuwa na mke, nabii, mwamuzi na kiongozi shujaa. Ushujaa wake ulitambulika na kila mtu hata Barak alikataa kwenda vitani bila kuambatana na Debora.

Debora alitambua wito wake na alifahamu kuwa aliyemwita na mkuu sana kuliko jemedari wa jeshi lolote au mfalme yeyote. Alijitoa kuwatumikia watu kwa kuamua matatizo yao kila siku, huku akiendelea na huduma ya kutabiri. Kazi ya kuamua matatizo ya watu inahitaji hekima na ufahamu wa hali ya juu, pia inahitaji kujitoa hasa kwa ajili ya wengine na kuwatanguliza. Debora alikuwa na sifa zote hizi na ndio maana watu walimwamini na kumtumia.

Mungu hutumia watu wenye moyo safi waliotayari kutumika kwa ajili ya kazi njema. Watu waliotayari kujikana na kujitolea kwa ajili ya kazi ya Mungu. Watu jasiri katika kufikisha ujumbe wa Mungu kwa watu bila kuangalia anaongea na nani.

Je, kwa kusoma sura hii umejifunza nini kuhusu Debora na mwanamke amchaye Mungu kwa ujumla?

Kitabu cha Esta

Esta 1-10

Somo. Esta 1-10

Ukisoma kitabu chote cha Esta utaona jinsi ambavyo esta alisimama katika nafasi yake katika kulitimiza kusudi la Mungu. Pamoja na kuwa mtoto yatima, hakuruhusu hali yake ya zamani iingilie kati katika ule mpango wa Mungu wa maisha yake.

Alikuwa mnyenyekevu na kusikiliza mashauri ya wale aliokuwa chini yao na kwa kufanya hivi aliweza kufanya maamuzi ya busara. Pale alipoona hofu, alifunga na kuomba na kisha kupata ujasiri wa kukabiliana na mambo makubwa magumu.

Katika kitabu cha esta tunajifunza mambo mengi, yakiwemo:
1. Kuwa wanyenyekevu na wasikivu kwa wale wanaotulea na kutuhudumia
2. Kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya watu wengine
3. Kufunga na kuomba pale tunapokabiliana na maamuzi muhimu ya maisha
4. Kutoka kwa mordekai tunajifunza kuwa tayari kuwalea na kuwahudumia ndugu zetu wanaoachwa na wazazi wao, kuwalea kama watoto wetu.
5. Kiburi hupelekea maangamizi
6. Ukiwa mwaminifu na kutenda mema hakika utalipwa usipozimia moyo
7. Maombi yanabadilisha msiba na maombolezo kuwa sherehe na vicheko.

Je wewe umejifunza nini baada ya kusoma kitabu hiki?

Wafilipi 4: Furaha na Amani

Shalom

Tunaendelea kujifunza kupitia kitabu cha wafilipi, leo ni sehemu ya nne. Kama haukuwa pamoja nasi anza kwa kusoma kitabu chote cha waraka wa Paulo kwa wafilipi kisha uangalie kwenye makala zilizopita usome sehemu ya kwanza hadi ya tatu halafu tuendelee.

Jambo lingine ambalo Paulo aliwaandikia na kuwasisitiza wafilipi ni kuhusu furaha ya kweli na amani ipitayo akili zote. Katika kitabu hiki tumeona jinsi yeye mwenyewe alivyoonyesha kuwa ni mtu mwenye furaha na amani ya kweli japo alikuwa kifungoni. Furaha ya Roho mtakatifu haiangalii unapitia nini wala nini kinakusonga, bali ukuu na uaminifu wa Mungu. Ipo juu ya hali zote, huangalia wokovu wa Mungu, rehema zake, upendo wake, Neno lake, uaminifu wake na uweza wake. Ni furaha inayotambua kuwa Mungu anafanya mambo yote kwa ajili ya kutupatia mema. Warumi 8:28-30. Furaha inayopatikana katika Yesu Kristo, katika maombi na katika imani kwa Mungu.

Unapokuwa na furaha ya aina hii ndipo unapoweza kupata amani ya Mungu ipitayo akili zote. Unatambua kuwa wewe huwezi kubasilisha hali yoyote bali kumkabidhi Mungu kila jambo naye atakuongoza juu ya kuliendea na kukushindia. Wewe usiangalie yanayokuzunguka wala kuyafikiria hayo kila wakati bali mambo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema, ukiwapo wema wo wote,  ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakari hayo.

Ubarikiwe na Bwana Yesu.

Wafilipi 3: Umoja

Wafilipi 2:1-4Basi ikiwako faraja yoyote katika Kristo, yakiwako matulizo yoyote ya mapenzi, ukiwako ushirika wowote wa Roho, ikiwako huruma yoyote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja. Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo  yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

Wafilipi 2:14-15 Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu.

Katika mistari hii tunaona ya kwamba Paulo alikuwa anawasisitiza watu wa filipi kuwa na umoja. Umoja ni nguzo muhimu sana katika ustawi wa kanisa. Mahali ambapo hapana umoja hapawezi kuwa na maendeleo maana chuki, fitina, magomvi na manung’uniko hutawala na watu hawawezi kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo iwe ni kiroho au kimwili. Sisi ni mianga katika ulimwengu, ulimwengu umejaa giza na kila mmoja huko hujishughulisha na mambo yake mwenyewe huku akiwakandamiza wengine. Inatupasa tuonyeshe mwanga wetu kwa kushikamana, kuwa na nia moja, kutangulizana na kufanya kazi ya Mungu pasipo manung’uniko wala mashindano.

Kuna watu wanafanya huduma ya Mungu kama mashindano, wanataka wao tu ndio waonekane kuwa wanamtumikia Mungu, akiinuliwa mwingine basi huanza kumuona kuwa hafai na hana thamani. Majivuno yamewafanya watu wengi washindwe kuziona nguvu za Mungu katika huduma zao na kubaki wakihudumu kwa mazoea. Mistari hii itufungue macho na kutambua kuwa sote tu watoto wa Mungu, tunafanya kazi kwa ajili ya ufalme na utukufu wa Mungu, hakuna haja ya mashindano wala majivuno.

 

Wafilipi – 2: Ukarimu

Matendo 16:13-15
Kutokana na kutokuwa na nyumba ya ibada katika Filipi, Paulo na wenzake walienda kusali kando ya mto na kuwahubiria wanawake waliokuwepo mahali pale. Mmoja wao aitwaye Lidia alipokea neno la Mungu na kuamua kubatizwa, kisha akawakaribisha nyumbani kwake. Baada ya hapo waumini wakawa wanakutanikia hapo.

Matendo 16:40 Nao wakatoka gerezani wakaingia nyumbani mwa Lidia; na walipokwisha kuonana na ndugu wakawafariji, wakaenda. zao.

Kanisa la Filipi lilianzishwa na Paulo kwa msaada wa ukarimu kutoka kwa Lidia aliyetoa nyumba yake iwe mahali pa kukutanikia. Ukarimu huu uliendelea na uliambukizwa kwa kanisa zima na waliendelea kumhudumia Paulo hata alipokuwa mbali nao.

2Korinto 11:9a Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu.

Filipi 4:18 Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafradito vitu vyote vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu.

Filipi 4:16 Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja.

Ukarimu huwa unaendelea na kuzaa ukarimu, ukarimu pia husimamisha huduma na huleta umoja. Tujifunze kuwa wakarimu kwa watumishi wa Mungu kama Lidia na kanisa la Filipi.

Wafilipi – 1: Utangulizi

Paulo aliuandika waraka huu kwa wafilipi:
1. Kuelezea shukrani zake kwa ushirika wao pamoja naye katika injili, imani aliyonayo kuwa watazidi kuendelea mbele, na kuzidi kustawi.
2. Kuwaelezea hali yake ya wakati huo, tumaini alilonalo na hofu yake.
3. Kuwasisitiza kuhusu kuwa na umoja, na unyenyekevu.
4. Kuwaeleza kusudio lake la kuwatuma kwao Timotheo na Epafradito.
5. Kuwaonya kuhusu watu wahubirio injili kwa ajili ya manufaa binafsi wautumainiao mwili.
6. Kuwasihi Euodia na Sintike wapatane.
7. Kuwatia moyo wawe na furaha siku zote, wadumu katika maombi na kutenda mema yote.
8. Kuelezea shukrani zake kwao kwa kujitoa kwa ajili yake.
9. Kuwasalimu

Unajifunza nini kutokana na haya?

Bible Study

image

Shalom

Weekend hii tujifunze biblia pamoja kwa kusoma kitabu cha wafilipi. Kaa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu ili uweze kupata mafunuo mbali mbali kisha tushirikishane hapa. Hakikisha unasoma kitabu chote kwa makini na kwa kujifunza.

Kutakuwa na majadiliano hapa kama una swali, neno la kutufaa au unahitaji ufafanuzi wowote. Karibu tujifunze biblia.