Thamani ya Mwanamke

Mungu aliona si vyema adamu aishi peke yake akaamua kumtafutia msaidizi wa kufanana naye. Wanawake tumeumbwa kwa kusudi kamili la Mungu na tunajukumu la kuwa wasaidizi. Nafasi ya mwanamke katika jamii, familia, ndoa, kanisa na taifa ni kubwa sana. Angalia jinsi wanawake wanavyohangaika na watoto, kuanzia wakiwa tumboni hadi wakiwa watu wazima. Mwanamke ni mjenzi wa familia, mwanamke ni muunganishi wa familia na mwanamke ni mrutubishaji wa familia.

Moyo wa mwanamke unauwezo mkubwa sana, yani hawa nakaa nafikiria moyo wa mwanamke nashindwa kuuelewa kabisa, wanawake wanatendwa kila siku lakini wanasamehe, wanajitahidi kuachilia japo ni ngumu na wanaamua kuendelea kutenda mema. Unakuta mama anagundua mumewe anatembea nje, na hata anafikia kulala nje, mama huyu atalia, ataumia lakini atampikia chakula, atamfulia, atamuombea ataamua kumsamehe na hata akiletewa mtoto wa nje  anamtunza. Hivi ni wanaume wangapi wanaoweza kuwasamehe wake zao wanaotembea nje? Na pale anaporudia na kurudia na wakati mwingine kulala nje???

Mungu awakumbuke wanawake wote.
Mungu asikie kilio chako unacholia ndani ya shuka na bafuni.
Mungu akuonekanie na kukurejeshea furaha ya maisha.
Mungu akutetee wewe ukiyepewa mimba na kuachwa.
Mungu akutunze wewe uliyetelekezwa na mume na ukaachiwa watoto.
Mungu awe mume wa wajane wote.
Mungu ailainishe mioyo ya waume wote, waitambue thamani ya wake walionao, Mungu awafunike macho yao wasione wengine zaidi ya wake zao.

Mungu alituumba kwa kusudi, tufurahie uanamke wetu na kamwe tusikubali changamoto za maisha zituondolee furaha. Mungu aliona dunia haitakuwa njema bila sisi ndio maana akaamua kutuumba, sisi ni wa thamani saanaaa….

Kusamehewa Sio Kibali cha Kuendelea na Makosa!

Kusamehewa hakukufanyi wewe uendelee na makosa eti sababu unajua kuwa utasamehewa. Unapoomba msamaha maanisha unachokisema na dhamiria kutoka moyoni kutokurudia tena kosa na epukana na mazingira yaliyokufanya ukatenda kosa hilo. Kuna watu kwa makusudi wanafanya makosa na kuyarudia wakijua kuwa wenzi wao watawasamehe sababu ni wepesi kusamehe. Unakuta mtu anafanya uzinzi, anasamehewa, anaendelea na wala hajali, au mtu anampiga mke wake, anasamehewa na anaendelea tena na tena.

Kusamehe hakumaanishi kuwa mtu upo tayari kuhatarisha maisha yako. Unaweza kumsamehe mtu anayekupiga lakini ukajitenga mbali naye sio sababu hujamsamehe bali kwa usalama wako watoto kama wapo na yeye pia maana anaweza kukudhuru akaishia gerezani, mpaka pale atakapoamua kweli kubadilika. Kusamehe hakumaanishi kuishi katika mateso.

Nawewe uliyesamehewa na kisha ukaendelea na makosa ukijua utasamehewa kumbuka ghadhabu wa Mungu ipo na hakika usipogeuka na kuiacha njia yako mbaya hauwezi kuiepuka!

Mwanandoa: Samehe!

Mwanandoa: Pale mwenzi wako anapokukosea kosa linalokuumiza sana, anapokutenda jambo ambalo hukutarajia na ni gumu sana kwako, hapo unapoona kuwa kila mtu atakuelewa kama ukiamua kuachana naye, unapoona unayo kila sababu ya kumlipizia, na unapoona kuwa huwezi kusamehe HAPO NDIPO UNAPASWA KUSAMEHE!!!

Kusamehe hakumaanishi kuwa ni rahisi kusamehe, kusamehe hakumaanishi kuwa  maumivu sio makali, hatusamehi kwa hajakukosea, kusamehe hakumaanishi kuwa umechangia kosa kutokea bali KUSAMEHE KUNAONYESHA JINSI UNAVYOMPENDA MWENZI WAKO, KUWA UPENDO WAKO KWAKE NI ZAIDI YA MAKOSA YAKE NA KUWA UNAMUANIMI MUNGU KUSHUGHULIKA NAYE NA KUMBADILISHA KABISA. Mwanandoa SAMEHE, haijalishi maumivu ni makali kiaso gani, amua kusamehe, na muombe Mungu akusaidie uweze kuachilia na kusahau kabisa maana ni kwa neema yake tu.

Mwanamke Mapishi

wpid-DSCN0996.JPG
Mwanamke ni lazima ujue kupika. Hakuna kisingizio kuwa nimesoma boarding tangu std one, mama hajanifundisha kupika, sina muda wa kupika n.k. Kupika kwa mwanamke ni heshima, ni sifa na ni wajibu. Kama unaweza kupata muda wa kuwa facebook basi unaweza kupata muda wa ku google mapishi mbalimbali na kujifunza. Sio rahisi ukapika kila siku lakini haifai mwanamke wiki nzima hujapika kabisa nyumbani kwako. Jitahidi kwa hali yoyote uwe ndio mpishi bora kuliko msichana wako wa kazi, hii inaleta heshima. Sio siku ukiingia jikoni watu wanatamani umwachie tu dada apike.

Jifunze mapishi mbalimbali kuanzia breakfast, appertizers, main course, soup, juices, disserts n.k. na kutoka maeneo mbalimbali yani Indian, Thai, American, Tanzanian n.k. Sio kazi ya siku moja lakini tangu unapoanza kujua kupika anza kijifunza kidogo kidogo, waweza weka ratiba kila mwezi unajifunza mapishi mapya mawili au moja baada ya mwaka utakuwa mbali sana. Tumia internet vizuri yaani itakufanya uwe chief cook hadi watu wa nyumbani kwako watamani uwapikie kila siku. Anza sasa, anza leo, anza usingoje kesho. Pia mnaweza kuwa mnajifunza pamoja na nashost wako wakaribu mara moja kwa mwezi badala ya kupiga tu story mkazipiga jikoni mkijifunza mapishi. Inasaidia sana kuboresha urafiki na kuongeza ujuzi.

Ndoa ni Zaidi ya Mapenzi

Mapenzi pekee hayatoshi kukufanya kuolewa au kumuoa mtu fulani. Unaweza kupendana na mtu, mkapendana kwa kasi yaani muda mfupi tu tangu mfahamiane mapenzi moto moto, kila dakika ni message, kila saa mnapigiana simu na kila wakati mnaonana. Unajiona yaani huwezi ishi bila yeye na unatamani mfunge ndoa hapohapo na kuanza kuishi pamoja. Wait…hapo sasa unahitaji speed gavana au wazungu wanasema reality check. Mapenzi ya msisimko kamwe sio kigezo cha kuwa na ndoa nzuri, sio kigezo cha kufunga ndoa maana hali hiyo ni ya msimu tu, siku mmeshaoana mnaishi pamoja na msisimko umeisha nini kitawaweka pamoja? Mmeokoka mnaona mnachelewa kujuana kiuhalisia hivyo ili msimkosee Mungu suluhisho mnaona ni ndoa, haya sasa mmeshaoana mmeshajuana weee na ule msisimko wa mwanzo umeisha, what next???

Ndio, lazima umpende mtu na mpendane ili muweze kuishi pamoja, lakini mambo haya ni ya muhimu kuzingatia kabla haujaamua kufunga ndoa. Je mtu huyo anaishi vipi na ndugu zake na watu wake wa karibu? Kadiri anavyoishi na ndugu zake ndivyo atakavyoishi na wewe baada ya msisimko kuisha. Je ni mtu aliyejaa malalamishi, ubinafsi, ubabe au mtu mnyeyekevu, mkarimu na mwenye kuwajali ndugu zake. Kama kwake kila ndugu yake na rafiki yake ni mbaya kasoro wewe, stop and think.

Je, anauhusiano gani na Mungu? Anauhusiano wake binafsi au tu kwa sababu wewe upo karibu na Mungu basi ili kukupata naye anajisogeza? Maisha yake ya binafsi yanamshuhudia vipi? Katika maongezi fahamu msimamo wake juu ya matumizi ya fedha, mahusiano na ndugu na pia mambo mbalimbali ya maisha. Halafu jiulize kama utaweza kuchukuliana naye na misimamo yake maana usijidanganye kuwa utambadilisha, ndoa ni kuchukuliana ila kila mmoja anamambo anayoweza kuyachukulia na asiyoweza.

Usifikiri tu kuwa sababu mnapendana basi mtafanana kwa kila kitu, hapana na ndoa inahitaji upendo, kuchukuliana, kujitoa, kusamehe, na kujali. Upendo usikufanye ukawa kipofu kwa mtu mwenye tabia ambazo hutaweza kuzichukulia kama ugomvi na kupiga, kukosa uaminifu, mdokozi, mbinafsi na mpenda makuu ambayo uwezo haupo.

Mwanamke Ishi Kwa Uwezo Wako

Shalom,
Wanawake wakati mwingine unaweza sababisha matatizo, majaribu na hata magonjwa ya moyo kwa mume na familia kwa ujumla. Wanawake tunapenda kupendeza, kuishi mahali pazuri, kula vizuri na kuonekana vizuri. Mambo haya sio dhambi ila hakikisha yanaendana na hali halisi ya maisha na kipato chenu. Kuna wanaume wana madeni kila benki, ofisini, marafiki n.k. kutokana na wake zao kulazimisha maisha ambayo ni juu sana na uwezo wao.

Mwanamke unatakiwa kujua jinsi ya kuipangilia nyumba yako na kuishi ndani ya uwezo wenu. Maisha ya kuiga na kutaka kuonekana uko juu hayatakufikisha mbali, utaibomoa nyumba yako kwa mikono yako mwenyewe. Kubali hali uliyonayo kisha fanya kazi kwa bidii ili kuiboresha na kufikia ndoto zako. Acha kulazimisha na kumpa mumeo pressure zisizo na msingi.

Ndoa ni Wajibu wa Wanandoa Wote

Wakati mwingine nikihudhuria kitchen party najihurumia ni vitu gani wasichana na wamama tunafundishana. Unakuta mwanamke anasimama na biblia anatuaminisha kuwa kutoka nje kwa mume sisi ndio tunasababisha kwa asilimia zote. Najua kila kitu kinakisababishi au kichocheo na mwanamke mpumbavu husababisha nyumba yake kubomoka lakini sio kweli kuwa sisi tuna ufunguo wa kumfunga asitoke nnje na kumfungua.  Wote tunajua kuna wamama wazuri wa nje na ndani, wanamcha Mungu na wanamaombi na kweli waume zao wanashuhudia ni wema na wenye kumudu majukumu yote katika ndoa hadi ya chumbani lakini bado waume zao wanatoka nje. Halafu akihudhuria mkutaniko wowote wa wanawake hasa wa kimungu anahukumiwa kuwa ukiona mwanaume ametoka nje basi ujue mkewe hamridhishi, mkaidi, mchafu, anakiburi n.k. Ina maana na mume akiwa akuridhishi, mkaidi, mchafu na mengine kama hayo mke nawe utegemewe kutoka nje???

Nijuavyo ndoa hujengwa na watu wawili waliokubaliana kupendana, kuheshimiana, kuchukuliana na kuishi pamoja siku zote katika hali zote. Kiapo cha ndoa kinasema …nitakuwa na wewe tu katika hali zote na wengine wote nitawaepuka… Ndoa hazisongi mbele sababu jukumu la kujenga na kusimamisha ndoa ameachiwa mwanamke pekee. Yani ndoa zaidi ya nusu zinaishi kutegemea moyo wa mwanamke, moyo wake wa kusamehe, moyo wake wa kumvumilia mume asiyetaka kubadilika, moyo wa kukubali lawama kwa kosa la mume na moyo wa kukubali kukaa na mtu anayetoka nje kila wakati ili tu watoto wawe na wazazi wote. Jiulize wanawake hawa wakichoka na kusema basi ndoa ngapi zitasimama.?? Je huu ndio mpango wa Mungu huu ya ndoa? Kwanini ndoa kwa wanawake ziwe msalaba na kwa wanaume kinga na kimbilio?

Mungu atusaidie wamama wenye watoto wa kiume tuanze kuwafundisha kweli ya Mungu, majukumu yao na wajibu wao wangali wadogo ili kuokoa ndoa zijazo. Kwa ndoa za sasa kweli waalimu wa wanaume na vijana wa kiume wanahitajika…kweli wanawake wametaabika vya kutosha…

Uaminifu Katika Ndoa

Uaminifu katika ndoa ni jambo la kila mmoja, sio la mke peke yake. Inashangaza sana kuona watu wakisema kuwa mwanaume hawezi kukaa bila kutoka nje sababu ndivyo walivyo. Kweli?? Hivi biblia kuna mahali inasema kuwa mwanaume ni kiumbe dhaifu? Nini tofauti kati ya mwanadamu na mnyama kama mwanadamu unasema ulishindwa kujizuia eti ni shetani. Yaani unakuta mwanaume katembea nje ya ndoa tena mara nyingine hadi kupata  mtoto akiulizwa anajitetea mara ni shetani, mara nilipitiwa mara mke wangu ndio kasababisha sababu ya hili na lile.

Halafu utakuta analazimisha mkewe amsamehe na haoni kwa nini ashindwe kumsamehe na kila mtu anamshangaa mkewe kwanini amsamehi wakati wanaume ndivyo walivyo na hata kumlaumu mke kuwa ndio sababu. Wakati mke akitoka nje ya ndoa hakuna anayetaka kusikia sababu yoyote tena hao wanawake wanaomlaumu mume akitoka nje ya ndoa ndio wanakuwa wa kwanza kumlaumu na kila mtu anamwambia mume muache huyu mwanamke hakufai. Hivi watu wanapoapa kuwa waaminifu mume huapa kuwa nitakuwa muaminifu kama mke akifanya hili na lile? Hivi wanaume hamuoni kuwa mnajidhalilisha kusema kuwa ulishidwa kujizuia? Ina maana hauna tofauti na jogoo anayemkimbiza kuku na kumaliza haja zake pale anaposikia hamu? Mtu utafute namba ya simu, muwasiliane, mkubaliane, utoke ulipo hadi gest upange foleni reception, upande ghorofani chumbani, uvue nguo bado tu unajitetea hukudhamiria, kweli? Huyo shetani alikufunga kamba?

Usidhani mkeo hapati vishawishi, tena inawezekana vikubwa kukushinda lakini aliahidi uaminifu kutoka moyoni sababu anakupenda na kumheshimu Mungu. Hakuna sababu yoyote inayoweza ku justify mwanandoa kwenda nje ya ndoa. Kila mmoja aheshimu viapo vya ndoa na kumuogopa Mungu. Hii ndiyo silaha pekee ya ndoa.

Timiza Ndoto Zako Sasa

Nirudi tena kwa wadada. Bado tupo na somo la mahusiano. Kuna wasichana wanafikiri maisha yao yataanza pale watakapoolewa. Unakuta mdada yupo tu wala hana malengo yoyote na maisha yake, mradi anafanya kazi basi yeye ni kula na kuvaa tu. Maisha unaanza pale unapozaliwa, haihitaji kuolewa ndio uwe na mipango ya maisha. Kuna walioolewa wakiwa na miaka kumi na kitu, wengine, ishirini, thelathini na pia wapo walioolewa wakiwa na miaka arobaini na kitu. Sasa kama unasubiri uolewe ndio uplan maisha yako unakosea sana. 

Lazima uwe na ndoto ni wapi unataka kufika, nini unataka kuwa nacho na kufanya kazi kwa bidii ili kuifikia ndoto yako. Unapoendelea kuitimiza ndoto yako Mungu atakukutanisha na mume wako huko huko na pamoja mtakuwa na mipango ya familia. Kama unandoto ya kuongeza elimu ifuate, iwe ni kufanya biashara, kufungua kampuni, kulima, kuwa muhubiri, muimbaji n.k. anza sasa kuitimiliza ndoto yako na umuombe Mungu akupe mtu ambaye kwa  pamoja mtatimiliza ndoto zenu.

Ukweli ni kwamba, kama sasa upo single na huwezi kuwa na mipango, ndoto na kufanya kazi kwa bidii, utakapoolewa na kuongezewa majukumu ya familia, na utakapopata watoto hutaweza kabisaa hata kuwa na hiyo ndoto. Tumia muda wako vizuri, tumia fedha zako vizuri na tumia vipawa vyako vizuri kuanzia sasa.

Mke Mwema Hutoka kwa Bwana…

Shalom

Kwanza nianze na vijana wa kiume. Misingi ya ndoa inaanzia kwenye mahusiano, lakini wakaka wengi siku hizi wamekuwa ni wavunja moyo sana. Ukijichunguza kwa makini utagundua ni wadada wengi sana umewavunja moyo na kuwaumiza. Unakuta kijana anaona ufahari kuwachumbia wadada zaidi ya mmoja na kisha kuwatosa, kuwachumbia na kuwatosa na wanapokuwa wanagombana kwa ajili yake anajiona kuwa ni mwanaume.

Leo unaona kama ni mchezo, na kweli wengi wanalia kwa ajili yako umewatosa baada ya kuwapa matumaini, lakini kumbuka apandacho mtu ndicho atakachovuna. Wasichana wanapolia kwa ajili yako umewatenda vibaya, maombi yao yanafika kwa Mungu na hakika atashuka kuwatetea. Kama huna mpango kwa kumuoa kwaninu kumdanganya na kumpa tumaini la uogo? Wengine mnawapanga makusudi kuangalia yupi bora, jamani mke sio bidhaa biblia inasema mke mwema mtu hupewa na Mungu. Acha kuwapanga wasichana badala yake nenda mbele za Mungu naye atakuonyesha yule mmoja ambaye ameandaliwa kwa ajili yako, aliye ubavu wako.