Loisi na Eunike

2 Timotheo 1:1-5 Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu, kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ikikaa kwanza kwa bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.

Hii ni mistari pekee katika biblia ambayo imewatambua Eunike na Loisi kwa majina yao. Loisi ni bibi yake Timotheo na Eunike ni mama wa Timotheo, mistari mingine inawaelezea ila si kwa majina yao.  Kwa muda mrefu Timotheo amekuwa msaidizi wa Paulo katika huduma yake. Paulo aliiona imani kubwa aliyonayo Timotheo na kutambua kuwa imetokana na malezi bora na mafundisho toka kwa mama yake na bibi yake. Aliwatambua wanawake hawa kama watu imara katika imani na katika malezi pia.

Matendo 16:1-3 Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke myahudi aliyeamini; lakini baba yake alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vyema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo alimtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni myunani.

Mama yake Timotheo, Eunike alikuwa ameolewa na mtu wa mataifa  na kutokana na kumheshimu mume wake hakimtahiri mtoto wake kama imani yake inavyosema. Hapa inaonyesha jinsi gani alikuwa mnyenyekevu na mwenye hekima. Pia Eunike alitambua kuwa pamoja na kwamba mtoto wake hakutahiriwa kama ilivyo desturi ya wayahudi, bado yeye analo jukumu la kumfundisha kweli ya Mungu tangu akiwa na umri mdogo. Alifanya hivi huku alipata ushirikiano toka kwa mama yake Loisi na kwa pamoja walimjengea Timotheo msingi imara wa imani.

Matendo 16:2 Mtu huyo alishuhudiwa vyema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio

Mistari hii inatuonyesha pia kuwa wanawake hawa hawakusimama peke yao bali walikuwa bega kwa bega na kanisa la Mungu. Timotheo hakupata mwongozo wa kiroho kutoka kwa baba yake maana hakuwa mwamini lakini mama yake alihakikisha anamuweka karibu kabisa na watumishi wa Mungu, waamini wa mahali pamoja ili waweze kuwa msaada kwake.

Tunajifunza kuwa sisi wanawake tunawajibu mkubwa sana katika kuwafundisha watoto wetu misingi ya neno la Mungu na wokovu. Ni muhimu sana hasa pale ambapo mwenzi wako hajaokoka maana Mungu anakuangalia wewe kuweka misingi bora ya kiMungu ndani ya moyo wa mtoto wako. Usipofanya hivyo shetani atapanda pando lake ambalo itakuwa ni ngumu sana kuling’oa.

Ubarikiwe na Bwana Yesu.

4 thoughts on “Loisi na Eunike

  1. Ubarikiwe dada, siku zote nashauri tupende kujifunza kwa watu waliotangulia. kama walifanya vibaya basi tusijunze kwanini yalitokea hivo na jinsi ya kuepuka. Pia kama walifanikuwa, tuiige imani yao ili tulifikie lile kusudi la Mungu.

  2. Wanawake ni watumishi wa mungu tunaihitaji kuwatia moyo/tusiwaache,tuwahimize ,tusiwaache hivyo

  3. je kuna wanawake wenye sifa kama za hawa wenye maadili mfano kwa siku hizi?

Leave a comment